Serikali yaunganisha  benki zake

17May 2018
Beatrice Shayo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Serikali yaunganisha  benki zake

SERIKALI imeziunganisha benki zake za  Twiga Bancorp Ltd na Benki ya Posta Tanzania (TPB) kuwa benki moja kuanzia leo, kwa lengo la kuongeza ufanisi.

Naibu Gavana wa Benki Kuu (BOT), Bernard Kibese, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu uamuzi wa kukubali kuunganishwa kwa benki za serikali za TPB na Twiga kuwa moja kuanzia leo. PICHA: HALIMA KAMBI

Aidha, benki binafsi ambazo zinataka kuungana, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezishauri kuiga mfano wa serikali ili kuleta ufanisi katika taasisi za kifedha nchini.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Gavana wa BoT, Dk. Benard Kibese, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kuunganishwa kwa benki hizo, ambapo alisema muunganiko huo umelenga kuimarisha utendaji na ufanisi kwa benki za serikali.

“Huu ndio mwelekeo wa serikali, imependa kuziunganisha benki zake ili kuwapo na benki moja yenye nguvu na benki ya TPB ina mtaji wa kutosha na inatii matakwa ya kisheria, sio kwamba imetetereka, wana mtaji wa kutosha kwa mujibu wa sheria. Pia madeni yote ambayo yalikuwa Twiga Bancorp Ltd yatakuwa chini ya benki ya TPB,” alisema Dk. Kibese.

Aliongeza: “Nadhani mnakumbuka Rais John Magufuli amekuwa akisisitiza haja ya kuwa na benki chache hasa zinazomilikiwa na serikali zenye kuleta ufanisi na kuchangia kwenye pato la taifa.”

Alisema benki ambazo zinamilikiwa na serikali zitarajie huo ndio mwelekeo na mchakato bado unaendelea, hivyo serikali haitasita kuziunganisha hizo benki ili kuleta ufanisi.

Aidha, alisema BoT kwa mamlaka iliyopewa chini ya Sheria ya mwaka 2006 namba 56 (1) na namba 56(a) hadi (d) Oktoba 28 mwaka 2016 iliiweka chini ya usimamizi Twiga Bancorp.

Alisema hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na benki hiyo kuwa na upungufu mkubwa wa mtaji kinyume cha matakwa ya sheria ya benki na taasisi za fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake.

Dk. Kibese alisema katika jitihada za kuboresha utendaji na ufanisi wa benki zinazomilikiwa na serikali, serikali ikiwa mmiliki mkubwa wa Twiga Bancorp imeamua kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa benki hiyo kwa kuiunganisha TPB.

“Hakuna kilichopotea ndio maana tumesema wateja, wafanyakazi, mali na madeni yote ya benki ya Twiga yatahamishiwa katika benki ya TPB,” alisema Kibese.

Dk. Kibese alisema muungano huu umeifanya BoT kusitisha usimamizi wa Twiga na masuala yote kuhusiana benki hiyo yatafanywa na TPB.

Alisema BoT inawaomba wateja wa Twiga kuwa watulivu katika kipindi cha uunganishaji wa benki hizo na kuendelea kupata huduma za kibenki kwa utaratibu utakaotolewa na menejementi ya TPB.

Nae Meneja Mwendeshaji wa Bodi ya Bima, Rosemary Tenga, akijibu swali la hatua zilizochukuliwa kutokana na benki tano zilizofutiwa umiliki wa leseni tangu Januari 4 mwaka huu, alisema wapo katika zoezi la kupata hali halisi ya mali na madeni ya benki hizo, ambapo lisema wanafanya ukaguzi wa hali halisi na shughuli hiyo itakamilika mwishoni mwa mwezi ujao.

Alisema baada ya shughuli ya ukaguzi wa benki hizo wataendelea na hatua ya kuuza mali ili kupata fedha za kuwalipa wadai na kama zitabaki fedha watalipwa wanahisa kwa mujibu wa sheria ya benki na taasisi za fedha.

Habari Kubwa