Serikali yaziondoa wasiwasi NGO 

17Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Serikali yaziondoa wasiwasi NGO 

MSAJILI na Mkurugenzi wa Idara ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Vickness Mayao, amewatoa hofu wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO) -

Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Baraka Leonard (wa pili kushoto) akifafanua jambo kwa mdau.

- kuwa serikali haina nia mbaya na mashirika hayo ila inataka uwapo  utaratibu mzuri wa kuyaratibu. 

Aliyasema hayo jijini Dar Es Salaam wakati alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na zoezi la usajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali linaloendelea jijini Dar es Salaam kwa Kanda ya Mashariki.

Alisema kuwa utaratibu wa usajili umerahisishwa sana hasa ule wa mashirika yaliyokuwa yamesajiliwa katika sheria nyingine.

Aliongeza kuwa wadau wameridhishwa na huduma zinazotolewa na ofisi yake na kusema wanapata mrejesho mzuri kutoka kwa wadau kupitia fomu za mrejesho wa zoezi hilo.

Mdau kutoka Taasisi ya Solidame Ifakara, Ali Mzava, alitoa rai kwa wadau wa mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyosajiliwa chini ya sheria nyingine kujitokeza kwa wingi kujisajili chini ya Sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali kwa kuwa usajili umeboreshwa na hakuna tatizo lolote katika zoezi hilo.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Tanzania Community Development Assistant, Denis Muchunguzi, alisema  wadau wameyapokea vizuri mabadiliko ya Sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali Na. 3 ya Mwaka 2019 kwa kuwa wameitikia wito na kujitokeza kwa wingi na hawana tatizo na utekelezaji wa marekebisho ya sheria hiyo.