Shein: Kuna wafanyabiashara wanaokwepa kodi Zanzibar

12Jan 2017
Mwinyi Sadallah
Nipashe
Shein: Kuna wafanyabiashara wanaokwepa kodi Zanzibar

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema bado kuna wafanyabiashara wanaokwepa kodi na kuikosesha serikali mapato wakati ni kinyume cha sheria.

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.

Alisema hayo alipokua akizindua tamasha la tatu la biashara linaloendelea katika viwanja vya Maisara ikiwa shamrashamra za maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Shein alionya kuwa, serikali itamchukuliwa hatua kali mfanyabiashara yeyote atakayebainika kufanya udanganyifu wa kukwepa kulipa kodi na ushuru na kuwataka watendaji kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wafanyabiashara hao.

“Bado kuna wafanyabiashara wanakwepa kodi na ushuru na kufanya vitendo vya udanganyifu kupandisha bei hasa wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani,” alisema.

Aliwataka viongozi na watendaji wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko Zanzibar kuendelea kulifanya tamasha hilo kila mwaka kwa vile lina umuhimu mkubwa katika kuimarisha na kuinua sekta ya biashara visiwani humo.

Aidha, Rais Shein alisema serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuimarisha wajasiriamali Zanzibar kutokana na kuwa na mchango mkubwa katika sekta ya uzalishaji na kuwataka kutumia masoko ya ndani na nje kutangaza bidhaa zao.

Alisema serikali imeamua kuondoa mfumo wa urasimu wa utoaji wa leseni za biashara na kuweka utaratibu mpya ili kuwaondolea usumbufu wafanyabiashara na wawekezaji.

Katika kulinda viwango vya ubora wa vyakula, Rais Shein alisema serikali yake imeanzisha mfumo wa ukaguzi wa bidhaa zinazoingia nchini unaosimamiwa na Shirika la Viwango vya Ubora Zanzibar (ZBS).

Pia alisema katika kuimarisha sekta ya biashara na utalii, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza kuangalia uwezekano wa kuanzisha safari za majini kwenda Comoro, Mtwara, Mombasa hadi Msumbiji kwa kutumia meli yake ya kisasa ya Mv. Mapinduzi II visiwani humo.

Habari Kubwa