Shell yapiga jeki gari la wagonjwa hospitali mkoa

27May 2019
Na Mwandishi Wetu
LINDI
Nipashe
Shell yapiga jeki gari la wagonjwa hospitali mkoa

KAMPUNI ya gesi ya Shell Tanzania, jana ilikabidhi gari ya kubebea wagonjwa kwa Hospitali ya Sokoine, ambayo ni ya Mkoa wa Lindi.

Meneja Mkazi wa Kampuni ya Shell Tanzania, Axel Knospe
(wanne kulia), akimkabidhi kadi ya gari la kubebea wagonjwa
Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mjini, Shaidi Ndemanga ambaye aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa huo, Godfrey Zambi kwa ajili ya Hospitali ya Mkoa mwishoni mwa wiki. MPIGAPICHA WETU

Akipokea gari hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga, aliishukuru Kampuni ya Shell na kueleza kwamba kampuni hiyo imefanya jambo kubwa linaloweza kusaidia kuokoa maisha ya wakazi wa Mkoa wa Lindi.

 

“Tulikuwa na uhitaji mkubwa wa gari ya kubebea wagonjwa katika hospitali hii ya mkoa. Sasa gari tumeipata. Tunawashukuru sana,” alisema Ndemanga na kuahidi kulitunza gari hilo.

 

 “Tutahakikisha gari hili linatunzwa na linafanya tu kazi iliyokusudiwa,” aliongeza.

Amesema serikali inatambua mchango wa Shell katika kuisaidia jamii na kuongeza kwamba kampuni hiyo iko mstari wa mbele katika kufikisha kwa Watanzania aina mbalimbali za nishati mbadala.

Katika hafla hiyo, Meneja Mawasiliano wa Shell Tanzania, Patricia Mhondo, alisema Mkoa wa Lindi unaendelea kuwa na ongezeko la watu, pia mahitaji ya kiafya yanaongezeka.

“Tumetoa gari hii kwa kuzingatia haya yote,” aliongeza Mhondo.

Alisema Hospitali ya Sokoine inahudumia wagonjwa wengi na kwa hiyo mahitaji ya gari la kubebea wagonjwa ni dhahiri.

Habari Kubwa