Sheria mpya EA yakwamisha madereva malori

11Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Iringa
Nipashe
Sheria mpya EA yakwamisha madereva malori

MADEREVA wa malori yaliyokwama katika mizani ya Wenda baada ya magari yao kuonekana kuzidi uzito unaokubalika kwa mujibu wa sheria mpya mpya iliyotungwa na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa lengo la kulinda ubora wa barabara, iliyoanza kutumika Januari mwaka huu, wameiomba .........

serikali kuwaruhusu kuendelea na safari.

Wakizungumza na gazeti la Nipashe katika moja ya hoteli wanapojihifadhi, madereva hao walisema wamejikuta katika kadhia hiyo baada ya magari yao kushindwa kusafiri kwa wakati licha ya kujua uwapo wa sheria hiyo na muda wa kuanza kutumika.

Msemaji wa madereva wa kampuni ya usafirishaji mafuta ya State Oil, Abuubakar Msangi, alisema magari hayo yalipakia shehena ya mafuta kwa ajili ya kuyasafirisha nchini Zambia tangu Desemba 18 hadi 25, mwaka jana, lakini wakashindwa kuanza safari kwa wakati kutokana na kutokamilisha baadhi ya vibali ikiwamo vya TRA na Sumatra, hali iliyowafanya kuanza safari kwa kuchelewa.

"Hayo magari unayoyaona hapo kwa idadi yapo kama 15, tulianza kupakua mzigo bandarini tangu tarehe 18 hadi 25 mwezi uliopita, lakini kutokana na mambo ya sikukuu za mwisho wa mwaka tukajikuta tumechelewa kupata vibali na hivyo kuchelewa kuanza safari. Sasa kama unavyoona tumekwama hapa kwa sababu mzigo tuliopakia ulikuwa ni wa uzito wa sheria ya zamani na sasa sheria mpya imetubana," alisema Msangi.

Alisema kutokana na kosa hilo wameandikiwa faini, lakini hawana uhakika wa kuendelea na safari kutokana na utaratibu kutaka magari yanayozidisha uzito kulipa faini na kupunguza mzigo ili kufikia uzito unaokubalika kisheria, lakini kwa kuwa mzigo walioubeba ni mafuta taratibu za kupunguza mzigo huo njiani ni ngumu badala yake wanaiomba serikali kuwaruhusu kuendelea na safari.

"Hapa tulipo maisha ni magumu sana hatuna huduma ya chakula ya uhakika na magari yanazidi kujaa hivyo tunawezajikuta tumekuwa wengi kiasi cha kuanza kugombea huduma hizi ambazo hata hazitoshi. Lakini pia sisi tunafamilia na hii ni kazi yetu na kosa hili hatujalisababisha sisi wenyewe kama unavyojua sisi ni wafanyakazi tu, lakini mwisho wa siku kukwama huku sisi ndiyo tunaopokea hii adhabu," alisema Msangi.

Mmoja wa madereva anayetoka nchini Zambia, Ismail Mshana, alisema alivuka na lori hilo Desemba 29, akitegemea kufikisha mzigo huo kabla ya kuanza kwa matumizi ya sheria mpya kuanza, lakini kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake amejikuta akikwama baada ya mzigo aliobeba kuzidi uzito unaokubalika na sheria hiyo mpya iliyotungwa na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa lengo la kulinda ubora wa barabara.

Mkurugenzi wa kampuni ya usafirishaji mafuta ya State Oil, Anil Nilesh, alipotafutwa na Nipashe kuelezea sakata hilo, kwa njia ya simu alisema bado wanaendelea kushughulikia suala hilo, lakini hawajaona sababu ya kutozwa faini hiyo kwa kuwa shehena hiyo ilipakiwa kwenye magari yao kabla ya muda wa sheria hiyo ndiyo maana magari hayo yaliruhusiwa kupita kwenye mizani ya Mikese na Mikumi.

Akijibu malalamiko na maombi hayo Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads), Mkoa wa Iringa, Mhandisi Daniel Kindole, alisema wamekamata magari ya kampuni ya State Oil pamoja na mengine kutokana na matakwa ya sheria mpya inayodhibiti uzito wa mizigo barabarani na kwamba wamekwisha waandikia faini, hivyo ni vema wahusika wakalipa faini kwa mujibu wa sheria ndipo waanze kupeleka maombi yao badala ya kuendelea kulalamika.

Nchi za Afrika Mashariki zilipitisha sheria ya pamoja inayosimamia uzito wa mizigo inayopitishwa kwenye barabara za nchi zao mwaka jana na kutoa kipindi cha miezi mitano ya maandalizi kwa wasafirishaji na wadau kujiandaa kwa matumizi ya sheria hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wadau juu ya utendaji na matumizi ya sheria hiyo mpya.