Shirika la Atomiki laahidi ushirikiano kuleta maendeleo

16Mar 2019
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Shirika la Atomiki laahidi ushirikiano kuleta maendeleo

MKURUGENZI wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) Kanda ya Afrika, Profesa Shaukat Abdulrazak, amesema wanatarajia kuongeza ushirikiano ili kutoa mchango zaidi katika kukuza maendeleo ya sekta mbalimbali Zanzibar.

Profesa Shaukat alieleza hayo alipofanya mazungumzo na uongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar ulioongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Asha Ali Abdalla, ofisini kwake Mnazimmoja.

Alisema lengo la kufika Zanzibar ni kukutana na watendaji wa sekta mbalimbali ili kuwaeleza juu ya nafasi kubwa iliyopo ya kuongeza ushirikiano kwa ajili ya maendeleo ya Zanzibar.

Alisema ushirikiano baina ya Shirika la IAEA na Tanzania ulianza tangu mwaka 1976 na linatoa ufadhili katika miradi mbalimbali inayohusisha sekta ya afya, kilimo, maji, mifugo, rasilimali watu, nishati na viwanda.

Kwa upande wa Zanzibar, Profesa Shaukat, alisema shirika hilo limesaidia katika kupambana na changamoto ya kuteketeza magonjwa yote yanayoambukizwa na ubongo na hivi sasa magonjwa hayo sio tatizo kubwa.

Alisema pamoja na kufadhili sekta mbali mbali, shirika hilo limeweka kipaumbele katika kuwajengea uwezo watendaji kwa kuwapa mafunzo ili kupata uelewa mpana zaidi katika kutekeleza majukumu yao.

Aliweka wazi kuwa Shirika la IAEA limeandaa mpango wa kuimarisha vitengo vinavyoshughulikia maradhi ya saratani katika hospitali zinazoshughulikia maradhi hayo baada ya kuonekana yanaongezeka kwa kasi katika nchi nyingi zinazoendelea.

Alisema kwa mujibu wa idadi ya Watanzania kunahitajika kuwa na mashine 55 zinazotoa huduma ya mionzi kwa wagonjwa wa saratani.

Aliongeza kuwa utafiti waliofanya wamegundua zipo mashine tano tu katika hospitali tatu zinazotoa matibabu hayo ikiwamo Ocean Road na Bugando Jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa mradi wa nguvu za atomiki duniani katika kanda ya Afrika unahusisha nchi 45, ambapo unajikita katika uhusiano wa ushirikiano katika nyanja tofauti.

Naye Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Dk. Jamala Adam Taib, aliueleza ujumbe huo kuwa serikali itajenga hospitali kubwa katika eneo la Binguni na kitengo maalum cha maradhi ya saratani kimepewa kipaumbele.

Alilishauri Shirika la IAEA kutoa msukumo zaidi suala la rasilimali watu na mafunzo kwa watendaji wa kitengo cha saratani, ili baada ya kukamilika Hospitali ya Binguni kuwe na nguvu kazi ya kutosha.

Akizungumza katika kikao hicho daktari wa huduma za Saratani Hospitali Kuu ya Mnazimmoja, Dk. Abdulrahaman Said, alisema kitengo kinachoshughulikia maradhi hayo hivi sasa kina madaktari wawili na wengine watatu wapo masomoni na miaka michache ijayo kitaimarika kufikia madaktari watano.

Alisema hivi sasa kitengo kinatoa huduma ya dawa na upasuaji tu kwa vile hawana mashine ya mionzi kwa wagonjwa wa maradhi hayo na hulazimika kuwapeleka Hospitali ya Ocean Road Dar es Salaam.

Habari Kubwa