Shirika lapeleka miche parachichi kwa wananchi

13Oct 2021
Anjela Mhando
Siha
Nipashe
Shirika lapeleka miche parachichi kwa wananchi

BAADA ya mahitaji ya parachichi kuongezeka katika soko la dunia, Shirika lisilo la kiserikali la Matonyok Organization linalojishughulisha na kilimo na utunzaji wa mazingira, limeupeleka mradi huo kwa wananchi wa Kata ya livishi, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro.

Shirika hilo limeanza kutoa miche ya parachichi bure kwa wakulima, kwa ajili ya kuwasaidia kuinua kipato chao, badala ya kutegemea zao moja la chakula.

Mkurugenzi wa Matonyok Organization, Alais Momoi, alisema katika kijiji hicho wanakusudia kugawa miche 100,000 kwa wakazi wake, baada ya kuona fursa katika kilimo cha Parachichi ndani na nje ya nchi.

“Mti mmoja wa Parachichi unatoa wastani wa kilogramu 150 hadi 500 na inakadiriwa kuzalisha Parachichi zenye thamani ya shilingi 200,000 hadi shilingi 750,000 kwa mti wenye umri wa miaka mitano hadi 10.

“Kimsingi, miche ambayo tunaigawa ni ya kisasa na kitaalam huzaa baada ya mwaka mmoja na nusu hadi miaka mitatu. Uamuzi wetu huu utawasaidia wakulima kuwa na kipato cha kujikimu kimaisha. Kwa sasa, baadhi ya wakulima wamekuwa wakichukua miche na kwenda kuiuza kinyume na malengo ya mradi.”

Parachichi za kisasa ni pamoja na Hass, Fuerte, Ndabal, Booth, Etinger na Waisal. Aina hizi za parachichi hupendwa sokoni kwa kuwa zina kiasi kikubwa cha mafuta au siagi.

Tanzania, zao la Parachichi hulimwa zaidi katika Mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Kilimanjaro na Morogoro.

Diwani wa Livishi, Luka Nkini, akizungumza kwenye mkutano maalumu, kwa ajili ya kupokea mradi huo, alisema wananchi wake wanashauku kubwa ya kulima zao hilo, kuwa hivi sasa lina soko la uhakika.

“Kwa sasa lina soko kubwa ndani na nje ya nchi, hivyo wananchi hawana budi kuchangamkia fursa hiyo, ambayo ni sawa na kuongeza ajira kwa wananchi wa Siha.

“Mmeona wenyewe sasa kampuni nyingi zimekuja wilayani kwetu, kwa ajili ya kilimo cha parachichi na kusafirisha kwenda nje ya nchi na wameajiri vijana wengi na sisi tusikae kimya, tupokee mradi huu ni ajira tosha.”

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Livishi, Solomoni Nkini, alieleza kufurahishwa kwake na ujio wa mradi huo, kwenye kijiji chake.

Habari Kubwa