Shivyawata masharti mikopo kuangaliwa upya

29May 2020
Grace Mwakalinga
Mbeya
Nipashe
Shivyawata masharti mikopo kuangaliwa upya

SHIRIKISHO la Vyama vya Watu wenye Ulemavu (Shivyawata), Mkoa wa Mbeya limeiomba serikali kuangalia upya masharti ya utoaji mkopo wa asilimia mbili kutoka halmashauri ili kundi hilo linufaike na kumudu gharama za maisha hasa katika kipindi hiki cha janga la ugonjwa wa Covid-19.

Ombi hilo lilitolewa jana na shirikisho hilo wakati wakipokea msaada wa ndoo tano za kunawia mikono ili kukabiliana na janga la ugonjwa wa Covid-19 ambazo zilitolewa na Naibu Waziri wa Kazi, Vijana anayeshughulika na watu wenye ulemavu, Stella Ikupa.

Akizungumzia suala la mikopo kwa watu wenye ulemavu, Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona (TLB), mkoani humo, Joseph Mwandalima, alisema kipindi hiki cha janga la corona hali ya kiuchumi imekuwa mbaya kwao.

Alisema hata mikopo inayotolewa na halmashauri imewekewa masharti magumu hali inayosababisha kukosa sifa ya kukopesheka na kuiomba serikali kuangalia upya ni kwa namna gani watalisaidia kundi la wenye ulemavu kupata mikopo.

“Miongoni mwa masharti ambayo halmashauri zetu imeweka kwenye mikopo yao ni kwamba kila kikundi lazima wapate usajili na barua kutoka kwa watendaji wa vijiji, sisi wenye ulemavu tumetawanyika unashangaa wawili wako kijiji kimoja na wengine wako mbali sasa ni ngumu kuunganika kwa pamoja cha muhimu watuhimize tujisajili bila kujali tunatoka kijiji kimoja,” alisema Mwandalima.

Aliongeza kuwa hali ya sasa kiuchumi kwao ni mbaya kuliko ugonjwa wenyewe wa corona, lakini aliwahamasisha wenzake kuendelea kuchapa kazi kwa kufanya shughuli ndogo ndogo za kujiingizia kipato.

Mwenyekiti wa Shivyawata Mkoa, Luca Mahenge, alisema licha ya kuwapo kwa idadi ndogo ya waliopo au kufariki kutokana na janga la corona, haiondoi uhalali kwamba wako kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa kutokana na tatizo la ukosefu wa vifaa vya kujikinga.

Alisema msaada wa Naibu Waziri Ikupa ndio wa kwanza kuupata tangu janga hilo liripotiwe nchini, wadau na serikali imewasahau katika vita hivyo licha ya kuwa uhitaji bado ni mkubwa.

Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye Ulemavu (Chawata) mkoa, Jimmy Ambilikile, alisema msaada wa ndoo kwa ajili ya kunawa mikono utagawiwa katika kila ofisi ya chama cha watu wenye ulemavu na wanahitaji  dawa na sabuni za kunawia.

Aliwaomba wadau na serikali kuendelea kuwasaidia vifaa mbalimbali vya kujikinga kwa kuwa ndoo hizo hazikidhi mahitaji kutokana na kila wilaya kuhitaji vifaa hivyo.

Habari Kubwa