Shule binafsi zashauriwa kukatiwa bima kuzikinga majanga ya moto

21Apr 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Shule binafsi zashauriwa kukatiwa bima kuzikinga majanga ya moto

WAMILIKI wa shule binafsi na za umma nchini, wameshauriwa kuzikatia bima ili kunusuru hasara kubwa ambazo zimekuwa zikipatikana yanapotokea majanga ya moto.

Ushauri huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Masoko wa kampuni ya Bima ya Bumaco ya jijini Dar es Salaam,
Halilya Kwayu, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini humo jana.

Kwayu alisema baadhi ya shule zimekuwa zikikumbwa na majanga ya moto na kupoteza mali nyingi yakiwamo majengo ya madarasa, mabweni, ofisi za walimu na mali za wanafunzi, lakini kwa kutokuwa na bima, huishia kupata hasara.

Kwayu alitolea mfano wa Shule ya Sekondari Iyunga mkoani Mbeya ambayo baadhi ya mabweni yaliteketea kwa moto.

Vile vile alisema katika tukio la hivi karibuni ambapo maduka kadhaa yaliteketea kwa moto katika Soko la Kayanga lililoko Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.

Alisema majanga hayo ya moto mbali ya kusababisha huzuni kubwa kwa wamiliki, lakini pia hurudisha nyuma maendeleona kusababisha umaskini katika familia na jamii kwa ujumla.

Kwa msingi huo, imewashauri wamiliki wa shule pamoja na wafanyabiashara mbalimbali hapa nchini, kuhakikisha kwamba suala la bima wanalipa kipaumbele ili kunusuru hasara zisizo za lazima.

Aidha, kampuni hiyo imesema imejipanga kutoa elimu ya bima kwa Watanzania ili kukabiliana na majanga mbalimbali yatokanayo na moto, wizi na mafuriko ambayo huharibu makazi na mazao.

Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Ramadhan Mungi, alisema elimu ya bima ni muhimu kwa jamii.

Mugi alisema wananchi wengi hukumbwa na majanga ya aina mbalimbali kwa sababu hawajafahamu umuhimu wa kukatia bima biashara zao, majengo na bidhaa za aina mbalimbali.

"Upo umuhimu mkubwa kwa wananchi kuelimishwa umuhimu wa bima kwa kutumia makongamano mbalimbali," alisisitiza.

Habari Kubwa