Sido yaanza mkakati wa kufufua viwanda

09Jan 2017
John Ngunge
ARUSHA
Nipashe
Sido yaanza mkakati wa kufufua viwanda

SHIRIKA la Viwanda vidogo (Sido) mkoa wa Arusha limeanza kutekeleza mkakati wa kufufua viwanda na kuongeza tija na ufanisi.

waziri wa viwanda, charles mwijage.

Shirika hilo limeanza kutekeleza mikakati hiyo kupitia mpango wa Kaizen neno la Kijapani lenye maana ya mabadiliko bora na endelevu ambao uliletwa nchini na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (Jica) kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara mwaka 2012 na ulianza kama mradi wa mfano kwa mikoa ya Dar es Salam, Dodoma na Morogoro.

Akitoa mafunzo maalum kwa wenye viwanda mkoani hapa mwishoni mwa wiki, Meneja wa Sido Mkoa wa Arusha, Nina Nchimbi, alisema Kaizen ni dhana ambayo imekuja kufufua viwanda nchini.

Alisema viwanda vingi nchini vimekufa kutokana na kutokuwa na uelewa sahihi wa nini kifanyike ili kuviimarisha na kuinua ubora wa bidhaa zinazozalishwa.

"Dhana ya Kaizen ya uongezaji tija imekuja kama mkombozi katika uboreshaji wa viwanda vyetu na mwitikio umekuwa mkubwa kwa wamiliki wa viwanda kujifunza ili kuongeza tija."

"Changamoto wazipatazo wamiliki wa viwanda mkoani hapa zinafanana na zile wazipatazo wamiliki wa mikoa mingine kama Dar es Salaam, hali ambayo imefanya Sido mkoa wa Arusha kuanzisha kwa nguvu mafunzo hayo ili kuongeza tija, ubora na kupata ufanisi," alisema.

Nchimbi alisema Kaizen inagusa nyanja zote katika maisha, hivyo inaweza kutumika majumbani, ofisini na mahala pengine popote.

"Misingi ya Kaizen ipo kwenye uvumbuzi na ubunifu wa mawazo na maarifa na ushiriki wa watumishi wote hasa dhamira na msukumo wa menejimenti. Utekelezaji wake unahitaji ushiriki wa kila mtu ndani ya taasisi, shirika au kampuni, alisema.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walisema wamefarijika kupata elimu hiyo na wanatarajia kuongeza tija katika shughuli zao.

Agnes Kalukwa, ambaye anamiliki kiwanda cha kutengeneza sabuni za kuogea kwa kutumia mimea asilia cha Aga Natural Products kilichopo Kijenge mkoani hapa, alisema mafunzo hayo yamemwongezea maarifa ya kuzalisha bidhaa zake kwa ubora zaidi.

Habari Kubwa