Sido yawezesha mafundi

27Jun 2016
John Ngunge
Arusha
Nipashe
Sido yawezesha mafundi

Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) Mkoa wa Arusha limetoa vitendea kazi kwa vikundi vya mafundi mchundo 42 kutoka wilaya za Longido, Arumeru na Arusha Mjini.

Vifaa hivyo ni kwa ajili ya mafundi seramala, uashi ushonaji nguo, bidhaa za ngozi, pikipiki na baiskeli, magari, wachomeleaji na wachonga mbao na kwamba kati ya vikundi vilivyonufaika saba ni vya wanawake na 21 ni vya wanaume.

Katika hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika mwishoni mwa juma jijini hapa, Afisa Ufundi, Stephen Leyan kutoka Sido Mkoa wa Arusha, alisema vifaa hivyo vimetolewa kwa ushirikiano na Shirika la kujitolea la Tools for Self Reliance (TFSR) la Uingereza.

Alisema shirika hilo linakusanya vifaa visivyotumika Uingereza kutokana na kukua kwa teknolojia, lakini bado vikiwa katika hali nzuri na kuvituma kulingana na mahitaji ya mafundi.

Utoaji wa vifaa hivyo unafuatia kukamilika kwa mafunzo maalum Machi mwaka huu kuhusu wajasiriamali watakavyoweza kuanzisha viwanda vidogo.

Mafunzo hayo yalikuwa yakiendeshwa na maafisa kutoka Sido mkoa wa Arusha.

Akisoma risala katika hafla ya kupokea vifaa hivyo, fundi Raphael Simon alisema wanaishukuru Sidon a TFSR kwa kuwaona mafundi wadogo.

“Tunaamini baada ya mafunzo na sasa kupata vitendea kazi na hata kurasimisha biashara zetu tutakuwa kwenye nafasi ya kuwa na sifa za kuchukua zabuni za kazi mbalimbali katika halmashauri zetu,” alisema.

Akikabidhi vifaa hicho, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Wilson Nkhambaku, alisema ni lazima Watanzania waitikie wito wa serikali wa kukuza viwanda kwa kuwekeza kwenye viwanda kuanzia vidogo, vya kati na hata vikubwa.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa