SMZ kununua pilipili hoho kwa wakulima

10Oct 2019
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
SMZ kununua pilipili hoho kwa wakulima

WIZARA ya Biashara na Viwanda imesema kuanzia sasa Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC) litachukua jukumu la kununua zao la pilipili hoho kutoka kwa wakulima.

Hayo yalisemwa jana na Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda, Hassan Khamis Hafidh, wakati akitoa ufafanuzi kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhusu mikakati ya serikali ya kuimarisha mazao ya viungo nchini.

Hafidh alisema mazao ya viungo soko lake lipo la uhakika na kazi kubwa iliyopo sasa ni wakulima kuongeza bidii ya kuzalisha mazao hayo ikiwamo pilipili hoho.

Aliyataja mazao ya viungo ambayo soko lake ni la uhakika hivi sasa kuwa ni pamoja na pilipili manga, vanila na hiliki.

“Mheshimiwa Spika napenda kuwajulisha wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwamba tumepata soko la uhakika la kuuza bidhaa zinazotokana na viungo ikiwamo pilipili manga, pilipili hoho na vanilla,” alisema.

Kutokana na uhakika wa soko kwa mazao hayo, Hafidh aliwataka Wawakilishi kuwahamasisha wakulima vijijini kuongeza kasi ya uzalishaji.

Alisema tayari mradi wa kuzalisha pilipili kichaa huko Panga Tupu Mkoa wa Kaskazini Unguja umeanza kuleta mafanikio baada ya wakulima kuotesha ekari 15 za aina hiyo ya pilipili.

"Soko kubwa la mazao ya viungo lipo katika nchi za Bahari ya Hindi pamoja na Arabuni na sasa limepanuka hadi China," alisema.

Habari Kubwa