Soko Kuu Karagwe laungua tena

08Jan 2017
Lilian Lugakingira
Karagwe
Nipashe Jumapili
Soko Kuu Karagwe laungua tena

SOKO Kuu la Kayanga lililoko wilayani Karagwe, mkoani Kagera limeteketea kwa moto usiku wa kuamkia jana na kusababisha hasara kubwa.

Kuungua kwa soko hilo kumesababisha hali ya kutoelewana kwa wakazi wa eneo hilo, kutokana na kwamba hiyo ni mara ya pili kukumbwa na tukio hilo katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja.

Aprili, mwaka jana, moto uliteketeza vibanda 140 na sasa harakati za kulijenga upya zilikuwa bado zinaendelea.

Mpaka sasa chanzo cha moto huo bado hakijafahamika na vyombo husika vinaendelea na ufuatiliaji wa tukio hilo.

Mbunge wa Karagwe, Innocent Bashungwa, akizungumzia tukio hilo, alisema inawezekana kuna hujuma zinaofanywa na watu ambao hawajafahamika.

"Naungana na wananchi wanaodai kuwa hapa kuna hujuma zinafanyika. Ninachoomba vyombo vya usalama vilifanyie kazi suala hili maana hata likijengwa lingine bila kufahamu chanzo cha matukio haya, wananchi wanaweza kuendelea kupata hasara," alisema.Alisema kutokana na umuhimu wa soko hilo, baada ya kuungua mwaka jana, lilikuwa limeshatengewa Sh. milioni 240 kwa ajili ya kulijenga na kuwa la kisasa, kwa kuwa ni chanzo kikuu cha mapato kwa wana- Karagwe.

"Nimefanya mawasiliano na Mkurugenzi wa Maafa Taifa (Ofisi ya Waziri Mkuu), ili kuangalia ni kwa namna gani wanaweza kutatua changamoto hii, ambayo inazidi kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi," alisema Bashungwa.

Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wilaya ya Karagwe, Livingstone Nestory, alisema tukio hilo limesababisha hasara kubwa kwa wananchi hasa wanaofanya biashara katika soko hilo.

"Hili ni pigo kubwa si kwa wafanyabiashara pekee bali kwa wananchi wa Karagwe kwa ujumla, hivyo serikali iliangalie jambo hili kwa jicho la huruma, kwani wengi walikuwa wamekopa kwenye taasisi za fedha,” alisisitiza.

Alisema ni jambo la aibu kwa wilaya ya Karagwe kukumbwa na tukio kama hilo kwa kuwa mwaka jana moto uliunguza soko hilo na kwamba kama kuna hujuma zinafanywa dhidi ya wafanyabiashara, hatua kali zichukuliwe dhidi ya watu watakaobainika kuhusika.

Akizungumza katika eneo la tukio, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Karagwe (OCD), Mika Makanja, alisema Jeshi la Polisi limeimarisha ulinzi kwenye eneo hilo kwa kuwa mwaka jana kulijitokeza wizi wa mali zilizokuwa zimeokolewa kutoka kwenye vibanda hivyo, baada ya soko kuungua.

Makanja alisema uchunguzi wa kina utafanyika wa kubaini chanzo cha moto, lakini kwa sasa cha muhimu ni kuimarisha ulinzi ili usitokee upotevu wa mali zilizookolewa.

Mmoja wa wafanyabiashara wa soko hilo, anayeuza vitunguu, Selina Wllibard, alisema wiki iliyopita alichukua mkopo ili kuongeza mtaji na kuwa alikuwa amenunua vitunguu magunia matatu, lakini vyote vimeteketea kwa moto.

Tathmini ya hasara iliyojitokeza bado haijafanyika kwa kuwa viongozi wa soko na wale wa halmashauri walisema ni mapema na kuwa watatoa taarifa baada ya kufanya hivyo.

Habari Kubwa