Soko la kimataifa lanukia

28Mar 2018
Furaha Eliab
 NJOMBE
Nipashe
Soko la kimataifa lanukia

WAKULIMA wa parachichi mkoani Njombe wamefundishwa jinsi ya kutumia viuatilifu vya kiasili ili kuingia katika soko la kimataifa la kutokana na parachichi za Tanzania zinakomaa wakati maeneo mengine ulimwenguni zinakua bila kukomaa.

parachichi.

Mtaalamu wa kilimo cha parachichi, Rebecca Hepelwa, anasema wakulima wanatakiwa kunyunyizia parachichi wakati wa maua ili  kudhibiti wadudu waharibifu katika matunda kwa kutumia mchanganyiko wa mizizi na matunda ambayo huunda sumu ya asili isiyo na madhara.

Kwenye mafunzo kwa wakulima wa parachichi ya kisasa katika Kata ya Ulembwe ya Wilaya ya Wanging’ombe ambapo wakulima wanapewa vitu vya kutumia kutibu parachichi wakati yakiwa katika hatua ya matunda.

 “Ili mtu auze kwenye soko la kimataifa ni lazima bidhaa zake ziwe za kiasili na hazina kemikali na kemikali zinatokana na matumizi ya dawa za wadudu na mbolea za kisasa ambazo huondoa sifa kwenye soko la nje la parachichi,” alisema Hepelwa na kuongeza:

“Dawa ya wadudu ya kienyeji unachukua pilipili, kitunguu swaumu limau na tangawizi vinasaidia kuua wadudu au kusaga mwarobaini nayo pia maji yake ni dawa ya kuua wadudu waharibifu na kuweka weka samadi na mboji.”

Alisema parachichi za Tanzania hukomaa tofauti na maeneo mengine kama Afrika Kusini ambako kunazalishwa parachichi nyingi zaidi ulimwenguni.

Aliongeza kuwa parachichi za Njombe zimekubalika katika soko la kimataifa kwa sababu ya uasili wake wa kutotumia mbolea na dawa za kisasa ambazo zinadaiwa kupunguza thamani ya parachichi na kupunguza ubora kwenye soko la kimataifa.

Wakulima wanasema baada ya mafunzo wanatarajia kuhakikisha kuwa wanalima parachichi kisasa na kuuza katika soko la kimataifa na kuulinda ubora huo.

Merck Mhepera, mkulima wa parachichi anasema wamepatiwa hatua za kuzifuata wakati wa kuandaa matunda kutokana na maandalizi mazuri ya shamba ambayo wameelezewa na mtaalamu.

Mkulima mwenye shamba darasa, Obed Mgaya, alisema wakulima wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanatibu maua.

Alisema kwa mkulima atakayefuata kwa umakini maelekezo kwa mti mmoja wa parachichi anaweza kuvuna mpaka parachichi 300 ambapo huongezeka mwaka hadi mwaka ambapo kwa parachichi aina ya X-Ikulu ambayo huuzwa moja kwa Sh. 500 shambani.

 

 

Habari Kubwa