Soko la maziwa lasababisha hasara mabilioni h/shauri 2

26Jul 2021
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Soko la maziwa lasababisha hasara mabilioni h/shauri 2

HALMASHAURI za Rungwe na Busokelo zinapoteza zaidi ya Sh. bilioni 50 kila mwaka kutokana na maziwa ambayo wananchi wanazalisha kukosa soko, hivyo kumwagwa na mengine kuuzwa kwa bei ya hasara.

Aidha, inadaiwa kuwa kukosekana kwa soko la uhakika la maziwa hayo kumesababisha baadhi ya wananchi kuanza kuuza mifugo yao ili wawekeze kwenye shughuli zingine ambazo zinawalipa.

Mbunge wa Busokelo, Atupele Mwakibete, aliyasema hayo wakati wa kikao cha wadau wa maendeleo wa halmashauri zote mbili ambacho kililenga kutatua kero ya kukosekana kwa soko la maziwa.

Alisema maziwa hayo yanakosa soko kutokana na wilaya hiyo kutokuwa na viwanda vya kuchakata maziwa, hivyo akashauri watafutwe wawekezaji ambao watawekeza kwenye viwanda vya kuchakata bidhaa zitokanazo na maziwa.

“Baadhi ya wananchi wameanza kukata tamaa ya kuendelea kufuga, sasa ni wajibu wetu kuwatafutia wananchi wetu masoko ya uhakika, hapa tunamtegemea mnunuzi mmoja pekee ambaye yupo Iringa na asiponunua basi wananchi wanamwaga na ndio tunapata hasara,” alisema Mwakibete.

Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Dk. Vincent Anney, alisema ili kukabiliana na tatizo hilo wanakusudia kuwapa kipaumbele cha mikopo ya halmashauri wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambao wataanzisha viwanda vidogo vya kuchakata maziwa.

Aidha, alisema wadau walikubaliana kujenga viwanda viwili katika wilaya hiyo ambavyo kimoja kitakuwa Busokelo na kingine Rungwe ili visaidie kukabiliana na tatizo la ukosefu wa soko la maziwa kwa wananchi wa Wilaya hiyo.

Vilevile, alisema waliunda kamati maalumu ya kufuatilia na kujua soko la maziwa ili wananchi washauriwe vizuri na kwamba kamati hiyo pia itafanya kazi ya ufuatiliaji wa ujenzi wa viwanda.

“Wananchi wanafanya kazi kubwa na hakuna anayewalazimisha, wanazalisha mazao ya kilimo na wanafuga, lakini tatizo kubwa lililopo ni masoko, sasa hivi mwananchi wa Rungwe akitamani kula ‘Yogurt’ ni lazima anunuwe za ASAS ambazo zinazalishwa Iringa,” alisema Dk. Anney.

Alisema wilaya hiyo inawakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwenda kuwekeza wilayani humo, na kwamba maeneo ya kuwekeza yapo na wataandaa mazingira rafiki ya uwekezaji.

Baadhi ya wafugaji walisema kwa sasa wanamtegemea mwekezaji wa Kampuni ya ASAS ambaye alishapatiwa eneo la kujenga kiwanda kwamba yeye ndiye atakayekuwa mkombozi wao.

Mmoja wa wafugaji hao, Daniel Mwalwayo, alisema ambaye ni mkazi wa Kiwira wilayani Rungwe, alisema asilimia ndogo ya maziwa wanawauzia wapita njia ambao alisema huwa wanauza lita moja kati ya Sh. 1,000 na 1,500.

Alisema bei hizo haziendani na gharama wanazotumia kuitunza mifugo yao na hivyo baadhi yao wanakata tamaa.