Sokoni wafundwa uchaguzi viongozi

06Dec 2019
Peter Mkwavila
Dodoma
Nipashe
Sokoni wafundwa uchaguzi viongozi

OFISA Masoko wa Jiji la Dodoma, James Yuna, amewataka wafanyabiashara wa soko la samaki wabichi, matunda na mboga la Bonanza, kuchagua viongozi wabunifu wa miradi itakayowaongezea mitaji yao.

Alisema wafanyabiashara wanatakiwa kutowachagua viongozi wao kwa ushabiki ambao wanaweza kuleta matokeo ya kuchochea migogoro na kusababisha mgawanyiko kati yao na uongozi wa jiji.

Tahadhari hiyo ilitolewa na ofisa huyo alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa wafanyabiashara hao ulioitishwa kwa ajili ya maandalizi ya kuwachagua viongozi.

Akizungumza kwenye mkutano huo wa wafanyabiashara, aliwataka kuchagua pia viongozi wenye kutumia hekima na busara kwa lengo la kulisaidia soko hilo na wao wenyewe kiutendaji.

“Wengi watajitokeza kutaka wachaguliwe kwenye soko hili, kinachotakiwa kwenu nyinyi wafanyabiashara muwachague wenye kubuni miradi ili muongeze mitaji yenu na siyo kwa kuwachagua kwa ushabiki unaoweza kuhatarisha maisha yenu na biashara zenu,” alisema.

Hata hivyo aliwataka wafanyabiashara wanao jishughulisha na uuzaji wa samaki wabichi kuweka mazingira safi kwenye maeneo yao wanayofanyia biashara, ili kuepukana na magonjwa ya mlipuko ambayo yatatokea katika kipindi hiki cha mvua za masika.

Mwenyekiti wa soko hilo anayemaliza muda wake, Goya Magwai, alisema pamoja na changamoto nyingi zilizopo, lakini bado wanayo sababu ya kuishukuru serikali kutokana na juhudi zake ambazo hivi sasa zimeanza kuonekana.

Alisema changamoto ambazo zimeanza kutatuliwa ni pamoja na miundombinu ya mitaro, vyoo na ujenzi mkubwa unaoendelea wa eneo la kuuzia samaki wabichi ambalo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi pindi watakapobaki.

Naye Diwani wa Chamwino, Jumanne Ngende, alisema atashirikiana na jiji kuhakikisha kero zilizobaki zinatatuliwa ili kuendana na hali halisi ya makao makuu ya serikali.

Aidha, aliwataka viongozi watakao chaguliwa moja ya majukumu wanayotakiwa kuyafanya ni kuunga mkono juhudi za serikali zinazotekelezwa sokoni hapo pamoja na kuhakikisha kujiepusha na migogoro.

Habari Kubwa