Spika aitaka serikali kupitia tozo mizigo bandarini

11Jun 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Spika aitaka serikali kupitia tozo mizigo bandarini

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, ameitaka serikali kupitia upya vigezo vilivyowekwa kwenye mizigo inayopita Bandari kwenda Zanzibar kutokana na kulalamikiwa na wananchi ikiwamo wabunge.

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai.

Mwongozo wa tozo kifungu cha 29 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), tozo ya 'Wharfage' inatozwa kwa mizigo ya biashara yenye uzito zaidi ya kilo 21 au yenye zaidi ya mita moja ya ujazo (CBM) inayopita kwenye gati, jeti na maboya yaliyo chini ya TPA.

Kauli hiyo ya Spika imekuja baada ya kujibiwa swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Maryam Salum Msabaha, kudai kuwa kuna changamoto bandarini na kwamba hata kilo 10 zinatozwa fedha hali inayosababisha malalamiko kwa wananchi.

Mbunge huyo alihoji ni vigezo gani ambavyo vinatumika kwa mizigo ya biashara na mizigo binafsi kwa wasafiri.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa, alisema vigezo vipo mwongozo wa tozo TPA na kwamba tatizo linaonekana ni uelewa.

"Niwaelekeze Bandari watoe elimu ya kutosha kwa wananchi wanaotumia usafiri kwenda Zanzibar ikiwamo hili la uzito wa kilo 21 na kuendelea ndio unatakiwa kutozwa, sio nia ya serikali kuona wananchi wake wanalalamika," alisema.

Kufuatia majibu hayo, Spika Ndugai, alisema kama kweli kilo 21 ndio kiwango cha chini ipo haja kuangalia kwenye boti.

"Maana kilo 20 hata sanduku la mwanafunzi linazidi, hata baadhi ya mashirika ya ndege yanatoa zaidi ya kilo 20, sasa kwenye boti kilo 20 ni kidogo sana."

Aliongeza "Ipo haja ya kuangalia kama sio sheria ni kanuni tu...Mtu akibeba mihogo mitatu kilo 20 tu anakuwa ameshavuka kwa hiyo tuliangalie, hawa wenzetu wanaotoka Zanzibar wapate raha kidogo na imekuwa kero kwa wananchi serikali iliangalie hili."

Katika swali la msingi, Mbunge huyo alisema abiria wanaokwenda Zanzibar kwa boti hulipishwa ushuru wa Bandari kwa mizigo hata kama boksi la kilo 10 au kilo 20 za mchele kwa Sh. 9,750.

"Je, ni mizigo gani ambayo abiria anapaswa kulipia ushuru huo wa Bandari (Wharfage)," alihoji.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Kwandikwa alisema TPA huikusanyi tozo yoyote kwa abiria ambao wana vifurushi binafsi vyenye uzito au ujazo mdogo wanaotumia Bandari kwenda Zanzibar kwa boti eneo la 'Baggage room.

Aidha, alisema abiria wanaotumia Bandari kwenda Zanzibar kwa boti ambao hutozwa ushuru katika eneo la 'Bagage room' ni wale tu wanaokuwa na mizigo mikubwa tena kwa madhumuni ya kibiashara.

Alitoa wito kwa wateja wote wanaotumia Bandari kwenda Zanzibar kwa boti wahakikishe kuwa mizigo yao inapimwa kabla ya kupakiwa ili wajue uzito wake unaostahiki kutozwa ushuru.

Habari Kubwa