Stanbic Benki yaidai kampuni bil. 5/- za mkopo

19Jan 2022
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Stanbic Benki yaidai kampuni bil. 5/- za mkopo

TAASISI ya kifedha ya Stanbic Benki (T) Limited imeipeleka mahakamani kampuni inayojishughulisha na usafirishaji, Nam Enterprises Limited kwa madai ya kutolipa mkopo wa zaidi ya Shilingi bilioni tano.

Benki hiyo inaishtaki kampuni hiyo na wakurugenzi wake wanne baada ya kushindwa kulipa mkopo wa Dola za Marekani 2,479, 005.58.

Shauri hilo limeshasikilizwa na Jaji Haruna Songoro wa Mahakama Kuu, Kitengo cha Biashara, ambaye ameamuru kampuni hiyo na wakurugenzi waliodhamini mkopo huo kulipa fedha hizo.

Katika shauri hilo Jaji aligundua kuwa benki imethibitisha madai husika na kwamba kulikuwa na mkopo ambao haujalipwa na kuwataka wadaiwa hao kurudisha fedha hizo na kuwaamuru kulipa gharama za kuendesha shauri hilo.

Hata hivyo, kampuni na wakurugenzi hao walikimbilia Mahakama ya Rufani ambako waliwasilisha taarifa ya kukata rufaa na kufanikiwa kuomba kusimamisha utekelezaji wa hukumu hiyo.

Gavana wa Benki Kuu, Profesa Florens Luoga, hivi karibuni alitoa waraka akieleza kuwa baadhi ya benki na taasisi za fedha zimekuwa zikitoa mikopo bila kufuata taratibu na kusababisha mikopo isiyolipika (NPLs) katika sekta ya benki.

Alitaja tabia hiyo kuwa husababishwa na baadhi ya watumishi wasio waaminifu wanaoshirikiana na wakopaji. Benki Kuu ilieleza kuwa itawafungia watumishi waliohusika na kuwazuia kuajiriwa katika benki au taasisi yoyote ya fedha nchini Tanzania.

Kwa benki ambazo wafanyakazi wake wana NPLs na benki nyingine, Gavana wa Benki Kuu aliagiza taarifa zao ziwasilishwe Ofisi ya Marejeleo ya Mikopo kwa hatua stahiki.

Benki Kuu pia ilizitaka benki na taasisi za fedha kutotoa mikopo kwa wakopaji wasio waaminifu waliokopa kwa nia ya kutorejesha mikopo hiyo, au wanaotumia udanganyifu kukopa.

Alisema taarifa za wakopaji zinapaswa kuwekwa kwenye daftari maalumu ambalo litashirikishwa na benki na taasisi nyingine za fedha.

Wakati huo huo, kampuni inayodaiwa imepewa miezi mitatu ya kurejesha mkopo huo kabla ya maelezo yao kuingizwa kwenye daftari maalumu.

Benki Kuu ilifanya mapitio ili kubaini sababu kuu za mikopo chechefu katika sekta ya benki na kubaini kuwa watumishi wa baadhi ya benki na taasisi za fedha wanawajibika moja kwa moja kupitia utoaji wa mikopo bila kufuata taratibu ambayo ni sawa na kukosa uadilifu.

Kiwango cha juu cha mikopo chechefu ni miongoni mwa sababu kuu za viwango vya juu vya mikopo na inaweza kusababisha kuyumba kwa sekta ya benki.

Habari Kubwa