SUA ilivyopunguza tatizo ajira

16Jan 2018
Christina Haule
Nipashe
SUA ilivyopunguza tatizo ajira

CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeajiri wafanyakazi wapya 190 ikiwa ni sehemu ya harakati za kuziba pengo lililoachwa na wafanyakazi 205 walioondolewa kazini Julai mwaka jana kutokana na kuwa na vyeti feki na elimu ya msingi.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu SUA, Prof. Raphael Chibunda.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu SUA, Prof. Raphael Chibunda alisema hayo jana wakati akiwapokea wafanyakazi hao chuoni hapo.

Prof. Chibunda alimshkuru Rais John Magufuli kwa kutoa kibali cha kujaza nafasi hizo za ajira na kuweza kuziba mapengo hayo.

Alisema kuwa chuo hicho kilitoa matangazo ya ajira na kupata jumla ya maombi 6,000 na kwamba baada ya mchujo walipatikana waombaji 2,000 wenye sifa.

Alisema waombaji 2,000 hao waliingia katika mtihani wa kuandika na kubakiwa waombaji 397 ambao waliitwa kwa mahojiano ya ana kwa ana na kufanya nafasi 114 kuidhinishwa kama wafanyakazi wapya kuanzia jana.

Alisema wafanyakazi hao wapya ni wa kada za wahudumu 102, polisi (6), wahadhiri (20, kompyuta (1), opareta wa mashine upande wa kilimo (1) na walimu wawili.

Aidha, Prof. Chibunda alisema nafasi 76 zilizobaki mchakato wake bado unaendelea katika ngazi mbalimbali za utumishi ili kufikisha nafasi 190 zilizoidhinishwa na serikali kwa  SUA.

Prof. Chibunda aliwataka wafanyakazi hao wapya kuheshimu sheria na kanuni za kazi zilizopo. Pia aliwataka kutojihusisha na kashfa za kimitandao ambazo zinaweza kuleta picha mbaya kwa chuo hicho.

Alisema kwa kuheshimu sheria za kazi katika sekta ya umma wanaweza kutumia nafasi zilizopo kupeleka malalamiko yao kama vyama vya wafanyakazi badala ya kuyatupia kwenye mitandao kama facebook.

Alisema kufanya hivyo kutaleta si tu picha mbaya kwa chuo bali pia ni kukiuka Sheria ya Mitandao.

Alisema chuo kiliwahi kupokea kesi ya wafanyakazi kujihusisha na masuala ya kashfa kwenye mtandao na walichukuliwa hatua za kinidhamu.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa SUA (Taaluma) Prof. Peter Gilla aliwaasa wafanyakazi hao wapya kutumia vyema muda wa mwaka mmoja wa majaribio waliopewa ili baada ya mwaka kuisha wote waweze kuendelea na kazi.

Alisema kuwa upo uwezekano wa mfanyakazi akaishia kwenye majaribio na kujikuta akikosa kuendelea na ajira kama hatafuata sheria za kazi, ikiwemo kujituma kazini.

SUA mpaka sasa ina jumla ya wafanyakazi 1,514 wakiwemo wahadhiri 550.

Habari Kubwa