Taasisi ya Clinton, TADB kuinua zao la soya

26Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
Iringa
Nipashe
Taasisi ya Clinton, TADB kuinua zao la soya

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeingia katika ushirikiano wa kimkakati na Clinton Development Initiative (CDI), iliyo chini ya Shirika la Clinton Foundation, ili kutoa mikopo hadi Dola 500,000 (Sh. bilioni 1.15) kwa ajili ya kufungua mnyororo wa thamani wa zao la soya mkoani Iringa. 

Kutokana na randama ya maelewano iliyosainiwa na mashirika hayo mawili, ushirikiano huo unalenga kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa Vyama vya Msingi (AMCOs) 29 na kuwanufaisha wakulima 2,900 walio katika programu maalumu ya CDI ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji na upatikanaji wa masoko kwa zao hilo katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa.
 
“TADB inayo furaha kubwa kuingia katika ushirikiano huu, kwa sababu ni mara yetu ya kwanza kama benki kujihusisha na mradi katika mnyororo wa thamani wa zao la soya. Pia duniani na hapa nchini, kuna ongezeko mkubwa sana la uhitaji wa zao la soya kama nyongeza ya virutubisho katika chakula cha binadamu.

Kuna wakulima na wajasiriamali wadogo na wa kati, hasa wanawake, ambao wanajishughulisha na biashara hii. Pamoja na hayo, kuna uhitaji mkubwa pia wa soya kama kirutubisho katika chakula cha mifugo pia, hususan kuku,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine.
 
Aliongeza: “Ushirikiano huu hivyo unawezesha kuwa na mfuko maalum wa mtaji kwa ajili ya kusaidia viongozi wa wakulima, benki za kijamii katika vijiji ‘VICOBA’ na wanachama wa AMCOs ili waweze kupata mbegu kwa ajili ya kuzalisha mbegu bora zaidi ‘na mbegu zilizothibitishwa kuzalisha nafaka za soya. AMCOs hizi pia zitapata mikopo maalum kwa ajili ya kuwawezesha kununua mapema mazao ya soya na kuwaunganisha katika soko la soya baada ya mavuno.”
 
Naye Mkurugenzi Mkazi wa CDI, Monsiapile Kajimbwa, alisema: “Chini ya ushirikiano huu, CDI imechangia rasilimali kwa ajili ya kufanya mafunzo ya kifedha na maendeleo ya kibiashara ya kilimo, ambapo TADB itakopesha Dola 500,000 sawa sawa na Sh. bilioni 1.15, katika hatua tofauti wa muda wa ushirikiano huu.”
 
Kajimbwa aliongeza, ikiwa uwezeshaji huo utawaongezea kipato wazalishaji wadogo wa soya kwa sababu AMCOs zinazoshirikiana na CDI zina nafasi nzuri zaidi kuwahudumia wanachama wao.

“Kwa miaka mingi, tumefanikiwa katika maeneo ya kutoa mikopo ya pembejeo za kilimo na mikopo ya shughuli baada ya mavuno kupitia vyama vya msingi tunazoshirikiana nazo. Hivyo, huu ni muda muafaka wa kupanua ukubwa wa mradi huu hapa mkoani Iringa, alisema.
 
Meneja wa Umoja wa Ushirika wa Wakulima Iringa (IFCU), Tumaini Lupola, alisema hatua hiyo ni fursa kubwa kwa IFCU katika kusaidia vyama vya msingi kurasimisha uuzaji wa mazao katika masoko, hususan soya kwa ajili ya kuwanufaisha wanachama na wakulima wao.

“Mikopo hii itawanufaisha sana AMCOs katika kufanya ununuzi wa mapema wa zao la soya kutoka kwa wakulima wao, kukusanya na kuwauzia wanunuzi kwa idadi kubwa na viwango bora zaidi kwa namna bora zaidi.”