Taasisi ya Tulia yatoa mkopo bodaboda 21

30Jul 2020
Grace Mwakalinga
Mbeya
Nipashe
Taasisi ya Tulia yatoa mkopo bodaboda 21

TAASISI ya Tulia Trust imetoa mkopo wa bodaboda 21 zenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 50 kwa vikundi mbalimbali vya waendesha bodaboda katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya.

Akikabidhi mkopo huo jana, Meneja wa Tulia Trust Jacqueline Boaz, alisema ni utaratibu kwa taasisi hiyo kuendelea kuwasaidia wananchi wa Jiji la Mbeya kujikwamua kiuchumi hususani vijana.

Boaz alisema baadhi ya vijana wa bodaboda walianza na mkopo wa Sh. 200,000 baada ya marejesho kuwa mazuri walikopa Sh. 800,000 na kuwawezesha kupata fursa ya kukopa vyombo vya usafiri ikiwamo bodaboda na Bajaj.

“Kupitia Taasisi ya Tulia Trust tumewasaidia wananchi wa maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya kujikwamua na umaskini kwa kupata mitaji na kufanya shughuli za kuwaingizia kipato ndio maana siku hizi vitendo vya uhalifu viwamo wizi vimepungua kwa sababu watu wako bize kujitafutia ridhiki naamini tutaendelea kutoa mikopo ya fedha na vyombo vya usafiri ili vijana waweze kutimiza ndoto zao,” alisema Boaz.

Akipokea mkopo huo kwa niaba ya wanachama, Mwenyekiti wa Bodaboda jijini hapa, Aliko Fwanda, aliishukuru taasisi hiyo kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu ambayo imesaidia kumiliki pikipiki za kwao badala ya kuendelea kuendesha pikipiki za watu.

Mmoja wa wanufaika na mkopo huo, Paul Christopher, alisema wamekubaliana kurejesha mkopo huo kwa wakati ili kutoa fursa kwa wengine kupata fursa hiyo.

Vituo vilivyopatiwa mkopo huo na idadi ya bodaboda kwenye mabano ni Sae (5), Igawilo (6), Stendi Kuu (2), Mwanjelwa (1), Ilomba bodaboda (5) na Iyunga (5).

Habari Kubwa