Taasisi yawezesha wananchi teknolojia ya kisasa ufugaji

11Jan 2019
Ibrahim Joseph
Dodoma
Nipashe
Taasisi yawezesha wananchi teknolojia ya kisasa ufugaji

TAASISI ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI), imewezesha kaya 3,676 na vijiji 135 teknolojia ya kisasa kwa ajili ya kusaidia shughuli za ufugaji.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, picha mtandao

Hayo yalielezwa juzi na Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, Dk. Eligy Shirima, alipokuwa akitoa taarifa ya kiutendaji ya ofisi hiyo mbele ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, alipotembelea.

Dk. Shirima alisema jumla ya kaya hizo 3,676 na vijiji 135 zinazovizunguka vituo saba vya taasisi hiyo vimewezeshwa teknolojia bora ya ufugaji.

Alisema hayo yanatokana na mpango mkakati wa taasisi hiyo waliojiwekea ya kuwasaidia wananchi wa vijiji jirani kwa kuwapa mbinu bora za ufugaji mifugo na kuwawezesha teknolojia kutokana na utafiti wa eneo husika.

Dk. Shirima alisema mpango mkakati mwingine ni katika mikoa 22 na wilaya 84 ambazo zitatumika katika kuzalisha malisho ya mifugo na mbegu zake, kurasimisha mbegu aina tano, kuzalisha mbegu za mikunde kilo gramu 500, nyasi mbegu kilo 4000 pamoja na kuzalisha marobota 50,000.

Aliongeza kuwa mipango mikakati ya ndani ni kushirikiana na taasisi za utafiti na maendeleo za ndani na nje kuibua miradi ya kitafiti.

Aliitaja mipango mikakati mingine ya ndani ya taasisi hiyo kuwa ni kuendelea na uzalishaji wa mitamba wa maziwa hadi kufikia 3,000.

Alisema wataendeleza uzalishaji wa mbuzi wa nyama na maziwa hadi kufikia 15,000 kwa mwaka wa 2019/2020.

Aidha, alivitaja vituo saba vya utafiti vilivyopo hapa nchini kuwa ni Kongwa, Mabuki, Tanga, Mpwapwa, Naliandele, Uyole na West Kilimanjaro.

Kwa upande wake Waziri Luhaga Mpina alisema lengo la kutembelea ofisi hiyo ni kufahamiana na kujiridhisha kwa kazi zinazofanywa.

Habari Kubwa