Taasisi za fedha kuwainua wakulima wa korosho

07Apr 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Taasisi za fedha kuwainua wakulima wa korosho

Serikali imekutana na taasisi za kibenki na kukubaliana nazo kufungua akaunti ya pamoja kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wa zao la korosho ili kuinua kilimo cha korosho.

Makubaliano hayo yamefanyika leo jijini Dodoma kati ya naibu waziri wa kilimo, Hussein Bashe, na wawakilishi wa mabenki hayo huku lengo likiwa ni kuwawezesha pia wakulima kupata pembejeo kwa wakati.

Akizungumza na wandishi wa habari, Bashe amesema amefanya kikao na Benki ya Equity ambayo imeonesha wazi nia yake ya kuwainua wakulima huku akiongeza kuwa Benki zingine ambazo zimeonesha nia hiyo na kukubaliana ni pamoja na Benki ya NMB na CRDB.

"Kama mnavyofahamu kwa muda mrefu tumekua tukiangalia njia ambazo zitawawezesha wakulima wetu kupata pembejeo kwa wakati na kwa gharama nafuu, kwa muda mrefu mazao haya ya kimkakati kama Korosho mkulima anaenda Benki anakopa fedha kwa ajili ya kununulia pembejeo lakini anaenda Benki anakopa kwa riba iliyopo kwa wakati huo," amesema.

"Sasa sisi kama Wizara tulikubaliana tuje na mkakati wa kumpunguzia gharama mkulima kwenye sekta ya kilimo hivyo tumeona ili kuondoa changamoto hiyo tutumie chama kimoja cha ushirika katika kushughulika nazo," amesema Bashe.

Habari Kubwa