Tabora kupaishwa kiutalii

14Nov 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Tabora kupaishwa kiutalii

SERIKALI imesema itaongeza juhudi za kuuendeleza na kuutangaza mkoa wa Tabora kiutalii ili kuongeza mapato ya nchi.

Hayo yalisemwa bungeni mjini hapa jana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga alipokuwa anajibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mwanne Mchemba (CCM).

Katika swali lake, Mchemba alitaka kujua kama serikali ipo tayari kuutangaza mkoa huo kiutalii baada ya changamoto ya usafiri wa anga nchini kuwa imetatulika na hivyo kuwa na ndege za Shirika la Ndege (ATCL) zinazotua mkoani humo.

Katika majibu yake, Hasunga alisema nia ya serikali ni kuhakikisha wageni wengi zaidi wanatembelea mkoa huo kwa lengo la kukuza utalii na kuongeza pato la taifa.

Alisema kwa ufanisi wa utangazaji utalii wa mkoa huo, juhudi za utangazaji zinazofanywa zinahusu vivutio mbalimbali vikiwamo vya mambo ya kale.

Alisema juhudi hizo zinahusu utamaduni, wanyamapori, mazao ya nyuki na historia pana ya harakati mbalimbali za kijamii za nchi zilizofanyika mkoani Tabora.

Naibu Waziri huyo alisema moja ya eneo la utalii mkoani humo ni tembe lililokaliwa na Dk. Livingstone.

Alisema kuwa Dk. Livingstone ambaye alikuwa mpinga biashara ya utumwa kutoka Uingereza, alikalia tembe hilo mwaka 1871 akiwa njiani kuelekea Ujiji Kigoma.

Hasunga alisema eneo jingine la kitalii mkoani humo ni kituo cha njia ya kati ya biashara ya utumwa na vipusa vilivyopo Ulyankulu, eneo la Mtemi Mirambo na gofu la iliyokuwa hospitali ya kwanza ya Kijerumani mkoani humo.

"Tembe la Livingstone limekarabatiwa na kuna watumishi ambao wanatoa maelekezo kwa wageni wanaotembelea kituo hicho," alisema.

Aliongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2013 hadi 2017, kituo hicho kilitembelewa na wageni 1,642 na jumla ya Sh. milioni 2.29 zilikusanywa kutoka ndani na nje ya nchi.

Hasunga pia alisema Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere pia alisema Tabora, hivyo jambo hilo litafanyiwa kazi ili liwe sehemu ya utalii.

Habari Kubwa