Tabora yamwagiwa magari, vifaa tiba

27Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Tabora
Nipashe Jumapili
Tabora yamwagiwa magari, vifaa tiba

SHIRIKA la Care Tanzania, limetoa msaada wa magari manne ya kubebea wagonjwa na vifaa tiba vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh. milioni 600 ili kusaidia kuboresha huduma za afya mkoani Tabora.

SHIRIKA LA CARE

Madhumuni ya msaada huo ni kushirikiana na serikali katika kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga na kusaidia pamoja na huduma za usafiri kwa wagojwa wanaohitaji matibabu ya dharura katika ngazi za juu.

 

Msaada huo ulikabidhiwa juzi na Mratibu wa Mradi wa Afya ya Mama na Mtoto wa Mkoa wa Tabora (Tamani) kupitia Care, Flavian Majenga, kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri.

 

Alisema magari manne ni aina ya Suzuki yana thamani ya Sh. 184,678,396 ambayo yatapelekwa katika zahanati za Usinge wilayani Kaliua, Mibono wilayani Sikonge na mengine mawili kwa ajili ya zahanati za Goweko na Tura zilizoko Uyui.

 

Majenga alisema mradi wa Tamani unalenga kuchangia jitihada za serikali katika kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya ya mama na mtoto na kuongeza matumizi ya huduma kwa wajawazito.

 

Aidha, Majenga aliongeza kuwa shughuli zinazotekelezwa chini ya mradi wa Tamani zitachangia mafaniko ya Kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama katika maeneo yanayohusu huduma wakati wa ujauzito, kujifungua na baada ya kujifungua.

 

Alisema mradi huo unafanya kazi na serikali mkoani Tabora katika kuimarisha mfumo wa rufani kwa wajawazito na watoto wachanga kupitia usafirishaji kutoka zahanati kwenda ngazi za juu za matibabu.

 

Majenga alisema hii ni mara ya pili kwa Care kutoa msaada wa magari na vifaa tiba kwa kuwa katika mradi uliopita wa Tabora Adolescents and Safe Motherhood (Tabasamu) uliokuwa unafadhiliwa na serikali ya Canada kwa miaka mitatu kuanzia 2012, walitoa magari 16 ya kubebea wagonjwa kwa halmashauri zote za mkoa wa Tabora.

 

Mratibu huyo wa Care alisema sambamba na msaada huo wa magari, Care pia imetoa vifaa tiba aina mbalimbali vyenye thamani ya Sh. 424,174,650/= kwenye zahanati 165 na vituo vya afya 11 katika halmashauri zote mkoani Tabora.

 

Alisema vifaa hivyo vimepelekwa katika wilaya ya Sikonge kwenye zahanati 24 na vituo vya afya vitatu ambavyo vina thamani ya Sh. milioni 49.1, Urambo zahanati 20 na kituo cha afya kimoja vyenye thamani ya Sh. milioni 42.8, Kaliua zahanati 36 na vituo vya afya viwili vyenye thamani ya milioni 75.7 na Nzega zahanati 11 na kituo cha afya kimoja vyenye thamani ya Sh. milioni 62.9.

 

Majengwa aliongeza kuwa, Halmashauri zingine ni Nzega Mji vitapelekwa katika zahanati mbili na kituo cha afya kimoja vyenye thamani Sh. milioni 15.1, Manispaa ya Tabora zahanati 19 na kituo cha afya kimoja vyenye thamani milioni 46.3, Uyui zahanati 37 na kituo cha afya kimoja vyenye thamani ya Sh. milioni 43.5 na Igunga zahanati 16 na kituo cha afya kimoja vyenye thamani Sh. milioni 88.5.

 

Akipokea msaada huo, Mwanri alilishukuru shirika hilo na kushauri mashirika mengine kuendelea kusaidiana na serikali kuokoa afya za Watanzania wakimemo mama wajawazito na watoto wachanga.

 

Aliwataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wajamzito na watoto hawatozwi fedha wakati wa kupata matibabu.

 

Habari Kubwa