TADB, NFRA zawatangazia wakulima neema soko mahindi

21Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
TADB, NFRA zawatangazia wakulima neema soko mahindi

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), kwa kushirikiana na Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula (NFRA), wameingia makubaliano kuongeza thamani ya mnyororo wa thamani wa zao la mahindi kwa kuhakikisha wakulima wa zao hilo wanapata soko la uhakika ili waweze kunufaika na kilimo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine.

Akizungumza baada ya kumaliza kikao cha pamoja, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine, alisema wamekubaliana na NFRA kuhakikisha zao la mahindi linapata soko, jambo litakalompa uhakika mkulima kuendelea na kilimo cha zao hilo.

“TADB ilishatoa zaidi ya Sh. bilioni 3.4 kwa vikundi 22 vya wakulima katika kufanya kilimo cha kisasa cha zao la mahindi, hivyo kupitia kikao hiki tunawahakikishia wakulima wa mahindi soko la uhakika,” alisema Justine.

Alisema kwa msimu wa kilimo uliopita soko la zao la mahindi liliyumba, hivyo kupitia mazungumzo kati ya TADB na NFRA yataibua matumaini kwa wakulima wengi wa mahindi kwa kupata soko la bidhaa hiyo ambayo bei yake ilishuka kutokana na uzalishaji kuongezeka tofauti na mahitaji ya nchi.

“Pamoja na Shirika la Chakula Duniani (WFP) kununua zaidi ya tani 36,000 za mahindi bado shehena nyingi za mahindi zipo kwa wakulima, hivyo kama wadau wa sekta ya kilimo ni wajibu wetu kuhakikisha shehena hizo zinapata soko,” alisema.

Hivi karibuni, Rais John Pombe Magufuli alishuhudia utiliaji saini wa makubaliano Ikulu jijini Dar es Salaam kati serikali kupitia Wizara ya Kilimo na WFP kuhusu kununua kiwango kikubwa cha mahindi.

Justine alisisitiza kuwa ili kumfanya mkulima kuendelea na kilimo cha zao hilo ni lazima ahakikishiwe soko la bidhaa yake itakayompa hamasa ya kulima kwa tija ili aweze kupata mavuno kwa wingi na tija inayotakiwa sokoni.

“TADB itaanda mkakati wa pamoja na NFRA utakaoleta mabadiliko makubwa katika mnyororo wa thamani wa zao la mahindi nchini, hii ni kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika msimu wa kilimo uliopita ulifanya zao la mahindi kushuka thamani,” alisema Justine.

Aliongezea kuwa kupitia mikataba wanayoingia NFRA na wanunuzi kutoka nje ya nchi itatupa mwongozo wa kuhamasisha kilimo nchini kwa

kuwakopesha wakulima kupitia Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima wadogo (SCGS) katika kufanya kilimo chenye tija na kukidhi mahitaji ya soko.

Alisema lengo ni kuhakikisha bei ya zao hili sokoni inakuwa ya kumnufaisha mkulima kwa kipindi chote cha msimu hali itakayomfanya mkulima kurudisha fedha yake na kupata faida itakayomsababishia kufanya maendeleo.

“Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imejipambanua kuboresha mazingira ya wananchi wa hali ya chini wakiwamo wakulima, hivyo TADB kwa nafasi yetu tunaendelea kutekeleza azma ya serikali kwa kuboresha mazingira kwa wakulima nchini,” alisema Justine.

kwa upande wake Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Vumilia Zikankuba, alisema wamefanya mazungumzo mazuri na TADB ambayo yatawasaidia kama wakala katika kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha zao la mahindi linapata soko.

“NFRA imejipanga kupunguza utegemezi kwa serikali katika kufanya shughuli zake, hivyo tunashirikiana na wadau wa kilimo na taasisi za kifedha kama TADB kutuwezesha fedha zitakazotusaidia kuendesha shughuli zetu za uhifadhi wa mazao na kujenga masoko,” alisema Zikankuba.

Alisema kupitia mazungumzo yetu tunauhakika wa kupata fedha zitakazo

tuwezesha kununua mahindi kutoka kwa wakulima, hivyo kutoa uhakika kwa

mkulima kuwa soko la zao hili lipo na kama wakala tutajitahidi kuhakikisha tatizo la ukosefu wa soko unapungua au kuisha kabisa.

Habari Kubwa