TADB yajitosa vita ya corona

27Sep 2021
Beatrice Moses
Dar es Salaam
Nipashe
TADB yajitosa vita ya corona

 
KATIKA kuhakikisha afya ya wafanyakazi na  wadau wake zinaimarika sambamba na kujenga uchumi imara wa taifa, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeratibu na kutoa elimu ya Uviko 19 pamoja utoaji wa chanjo kwa wadau mbalimbali.

Mbali na wadau wamo pia wakiwamo wafanyakazi wa benki hiyo jijini Dar es Salaam.
 
Akizungumza kwenye uzinduzi wa zoezi hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege, alisema benki hiyo inaunga mkono juhudi za serikali kupambana na Uviko-19, jambo ambalo limeisukuma benki yake kushirikiana na JKCI kuratibu zoezi hilo kutoa fursa kwa wadau wake kupata elimu na chanjo sahihi ili kulinda nguvu kazi kwenye sekta ya kilimo ambayo imeajiri takribani asilimia 60% ya Watanzania wote.
 
“Leo tumepata wasaa mzuri wa kuendesha zoezi hili, lakini lengo hasa ni kuona elimu kuhusu janga hili la Covid-19 inawafikia wadau wengi na hata huduma ya kuchanja wanaipata hapahapa tena kwa wakati ili kuokoa nguvu kazi hii kubwa kwa taifa,” alisema Nyabundege.
 
Aliongeza: “TADB inatekeleza malengo ya serikali ya kuanzisha chanjo tembezi ambayo itaongeza idadi ya vituo vya chanjo kutoka vituo 550 hadi vituo 6,784 jambo ambalo linatoa fursa wafanyakazi na familia zao kupata huduma hiyo kwenye makao makuu ya ofisi hizo bila gharama zozote.”
 
Aidha, Nyabundege aliwahimiza wadau wa sekta ya kilimo nchini kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vilivyoainishwa nchi nzima ili waweze kujikinga na athari za ugonjwa huo ikiwamo kupoteza maisha.
 
“Kwa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), inasemekana mpaka sasa watu takribani 4,697,099 wamepoteza maisha kutokana na athari ya ugonjwa huu, hivyo basi kwa umuhimu mkubwa niwaombe Watanzania wenzangu kushiriki kikamilifu kupata chanjo ili tuondokane na hatari ya kupoteza maisha utakapopata ugojnwa huu,” alisema Nyabundege.
 
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Rashid Mfaume, alizipongeza TADB na JKCI kwa kuratibu zoezi hilo na kuwataka wadau mbalimbali nchini kuondoa dhana potofu juu ya chanjo ya ugonjwa huo.
 
Alisisitiza kuwa maendeleo yoyote katika taifa lolote yanaendana na uwapo wa nguvukazi yenye afya bora, hivyo wajitokeze kwa wingi kupata chanjo kwa faida ya familia yao na hata taifa.
 
Naye Mkurugenzi wa Kurugenzi wa Magonjwa ya Moyo kutoka (JKCI), Dk. Tatizo Waane, aliwahamasisha watu kujitokeza kuchanja kwa kuwa chanjo hiyo ni sawa tu na chanjo zingine ambazo zinatolewa kwa lengo la kudhibiti athari kubwa ya ugonjwa huo.

 

Habari Kubwa