TADB yawapa neema wakulima wa kahawa

07Dec 2018
Lilian Lugakingira
Karagwe
Nipashe
TADB yawapa neema wakulima wa kahawa

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imesema imejipanga kunyanyua kipato cha wakulima wadogo nchini kupitia ushirika wao kwa kuwapatia mikopo ya gharama nafuu, ili kumudu gharama za uzalishaji.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB, Rosebud Kurwijila, alipotembelea na kufanya mazungumzo na uongozi wa Chama cha Ushirika Karagwe (KDCU) mkoani Kagera, ili kujionea namna mkopo uliotolewa na benki hiyo ulivyosaidia katika ununuzi wa kahawa kwa msimu ulioishia Oktoba mwaka huu.

Alisema TADB imedhamiria na kujizatiti kuhakikisha inanyanyua kipato cha mkulima mdogo nchini, ili kubadilisha maisha yake kupitia vyama vyao vya ushirika.

Alisema tangu imeanzishwa wamekwishatoa mikopo ya Sh. bilioni 55, ukiwamo wa KDCU wa Sh. bilioni 14, na kuwa hawatoi mikopo kwa mtu au taasisi ambayo haionyeshi mpango wa namna gani wananchi waliomzunguka watanufaika.

“Nimefurahi kutembelea baadhi ya wateja wetu na kukuta fedha walizokopeshwa zimewanufaisha walengwa wa mkopo huu,” alisema.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa mbele ya Mwenyekiti huyo wa TADB, wakulima wa zao hilo katika Wilaya za Karagwe na Kyerwa wamefanikiwa kukusanya kahawa kilo milioni 39.4 zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 39.4, katika msimu wa mwaka huu.

Mwenyekiti wa KDCU, Anselimi  Kabateleine, alisema kiwango cha kahawa kilichokusanywa katika msimu huu hakijawahi kufikiwa tangu KDCU ilipoanzishwa na kuwa mafanikio hayo yamewezeshwa na mfumo wa sasa unaovipa vyama vya ushirika vya msingi nguvu za ukusanyaji kahawa.

“Tunaishukuru serikali kwa kubadilisha mfumo wa ukusanyaji wa kahawa, kwa sasa kahawa imekusanywa ya kutosha kupitia vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS), lakini tunaishukuru TADB kwa kutupatia mkopo wa Sh. bilioni 14 uliotuwezesha kuwalipa wakulima kwa wakati,” alisema.

Alisema katika malipo ya awali zimelipwa Sh. 1,000 kwa kila kilo moja ya kahawa na kuwa kwa sasa kuna kahawa kilogramu milioni tatu haijapata mnunuzi, ambayo ikiuzwa fedha zitakazopatikana zitatumika kuwaongezea wakulima malipo ya pili.

Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Deodatus Kinawilo, alisema serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na TADB katika kuinua wakulima hasa wa zao la kahawa, ambalo ni tegemeo kwa mkoa huo. 

“Maprofesa mnaowaona wanaotoka Mkoa wa Kagera wamesomeshwa na kahawa, kwa hiyo sisi kama serikali tunaahidi kuendelea kusimamia fedha zinazotolewa na TADB kuwezesha wakulima wa kahawa, ili kuhakikisha zinatumika inavyokusudiwa na kurejeshwa kwa wakati,” alisema.

Habari Kubwa