Tahadhari yatolewa ulaji nyama mbichi, maziwa yasiyochemshwa 

13May 2022
Stephen Chidiye
TUNDURU
Nipashe
Tahadhari yatolewa ulaji nyama mbichi, maziwa yasiyochemshwa 

UNYWAJI maziwa yasiyochemshwa na ulaji wa nyama zinazotokana na ndege ambazo havijaiva vizuri ni hatari kwa afya ya binadamu ikiwamo kuambukizwa magonjwa kikiwamo kifua kikuu (TB).

Mtratibu wa TB na Ukoma Wilaya ya Tunduru, Dk. Mkasange Kihongole, alisema hayo juzi wakati akizungumza na  wananchi waliojitokeza kupima afya ili kubaini kama wana maambukizi ya kifua kikuu, katika kijiji cha Muhuweni.

 

Dk. Kihongole alisema hali hiyo imetokana na kuwapo kwa taarifa za kitaalamu zilizothibitisha kuwa kuna aina ya ndege ambao huliwa na ng'ombe ambao hutoa maziwa na kutumiwa na binadamu, hivyo kuwapo uwezekano wa kupata TB kirahisi.

 

 

Kwa mujibu wa Dk. Kihongole, uchunguzi wa kitabibu unaonyesha kuwa asilimia 20 ya wagonjwa wa kifua kikuu huambukizwa kwa kutumia njia hizo huku asilimia 80 wakiambukizwa kwa njia ya hewa.

 

Kihongole alisema wazee, watoto, wanaotumia pombe kupita kiasi, wavutaji wa sigara na bangi, wako kwenye hatari kubwa kuambukizwa kifua kikuu sambamba na watu wanaoishi katika makazi duni na abiria wanaosafiri kwenye vyombo vya moto.

 

Alisema kutokana na uwapo wa viashiria hivyo miongoni mwa jamii inayoishi wilayani Tunduru, takwimu zinaonyesha kuwapo kwa idadi kubwa ya wagonjwa wa TB kwa kuwa katika kipindi cha mwaka 2021 pekee, ofisi yake ilibaini wagonjwa 765 katika vijiji vitano vilivyofanyiwa utambuzi.

 

Dk. Kihongole pia alisema kutokana hali hiyo, Wizara ya Afya ilianzisha Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma kwa kuanza kutumia kliniki inayotembea ikiwa ni jitihada za serikali kuwajali wananchi wake na kutokomeza.

 

Mpango huo, alisema  unakwenda sambamba na malengo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) yanayoelekeza kuwa ifikapo mwaka 2030 -2035 pasiwapo na TB na ugonjwa huo kubaki historia kama ilivyo kwa ugonjwa wa ndui ambao ulisumbua sana wakati wake.

Habari Kubwa