TAKUKURU Shinyanga yabaini madudu miradi minne ya maendeleo

20May 2022
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
TAKUKURU Shinyanga yabaini madudu miradi minne ya maendeleo

​​​​​​​TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Shinyanga, imebaini kuwapo na dosari kwenye ujenzi wa miradi minne ya maendeleo, kati ya miradi 18 ambayo imeikagua yenye thamani ya shilingi bilioni 13.7.

Mkuu wa Takukuru mkoani Shinyanga Hussein Mussa, amebainisha hayo leo wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa vyombo vya habari ya robo tatu ya mwaka wa fedha (2021-2022), kuanzia Januari hadi Marchi mwaka huu.

Amesema kwa kipindi hicho wamefanya uchunguzi kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo 18, ambayo inatekelezwa mkoani humo yenye thamani ya shilingi bilioni 13.7 ambapo kati ya miradi hiyo minne imekutwa na dosari, na kutoa ushauri ifanyiwe marekebisho ili iendane na thamani halisi ya fedha.

“Miradi minne ambayo tumeikuta ina dosari ni ujenzi wa shule ya Sekondari ya wasichana Butengwa msingi wake kujengwa chini ya kiwango, Shule ya Sekondari Usule haikujengwa miundombinu ya wanafunzi wenye ulemavu, na ujenzi wa barabara za Changalawe Manispaa ya Shinyanga kujengwa chini ya kiwango,” amesema Mussa.

“Mradi mwingine ambao tumebaini una mapungufu ni ujenzi wa kituo cha Afya Salawe, umekuwa na dosari kwenye upande wa manunuzi ya vifaa vya ujenzi na uchunguzi wake unaendelea,”ameongeza.

Aidha, amesema katika kipindi hicho Taasisi hiyo pia ilifanya kazi ya uchambuzi wa mfumo katika Manispaa ya Shinyanga kwa wakala wa huduma ya ununuzi Serikalini (GPSA), na wakala wa umeme na ufundi (TAMESA) na kuziba mianya ya Rushwa iliyobainika katika Taasisi hizo.

Katika hatua nyingi alisema katika dawati la uchunguzi wamepokea taarifa 48 za malalamiko, zinazohusu Rushwa ni 35 na nyingi 13 siyo za Rushwa, na kati ya taarifa hizo za Rushwa 35, taarifa 17 uchunguzi wake unaendelea, 13 uchunguzi umekamilika, Tano uchunguzi umefungwa kwa kukosa ushahidi, Nne zimehamishiwa idara nyingine, 9 zilitolewa ushauri.

Habari Kubwa