Takwimu kikwazo utengaji maeneo wafugaji

14Feb 2020
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Takwimu kikwazo utengaji maeneo wafugaji

UKOSEFU wa takwimu sahihi za mifugo kwenye vijiji kumetajwa kuwa moja ya sababu za Serikali za Vijiji kushindwa kutenga maeneo ya malisho yanayokidhi mahitaji ya wafugaji katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo kusababisha migogoro ya wafugaji na wakulima kuendelea.

Hayo yalisemwa na wadau wa mifugo mkoani Mbeya wakati wa mkutano wenye lengo la kujadili matatizo yanayoikabili sekta hiyo pamoja na njia za kuzitatua ili kuiendeleza kwa maslahi ya taifa.

Mkutano huo uliwakutanisha maofisa mifugo wa kata zote za Jiji la Mbeya, Watendaji wa Halmashauri na Maofisa kutoka katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbeya, Hassan Mkwawa, alisema takwimu za mifugo ni muhimu wakati wa kupanga matumizi bora ya ardhi katika eneo lolote nchini.

Alisema maeneo mengi kwenye vijiji yanatengwa kwa ajili ya mifugo, lakini baada ya muda yanaonekana ni madogo kutokana na kutengwa bila kuwa na takwimu sahihi ya mifugo ya maeneo husika.

“Sasa hivi maeneo mengi yananunuliwa na watu binafsi na hivyo kufanya maeneo yanayomilikiwa na vijiji kupungua, sasa ni vizuri tukawa na takwimu sahihi za mifugo ili tutatuwe tatizo hili la upungufu wa malisho,” alisema Mkwawa.

Alisema kitendo cha maeneo ya malisho kutotosheleza mahitaji ya mifugo ndio chanzo cha wafugaji kuingiza mifugo yao kwenye maeneo ya wakulima na hivyo kuzua migogoro ambayo imekuwa ikisikika katika maeneo mbalimbali nchini.

Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani kutoka katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Angelo Mwilawa, alisema wizara hiyo imejipanga kutoa elimu kwa wafugaji ili wafuge kisasa na kwa tija kuliko ilivyo sasa.

Alisema lengo la elimu hiyo ni kutaka wafugaji wafuge mifugo michache ambayo inaendana na malisho yaliyopo badala ya kufuga mifugo mingi ambayo inakuwa haina ubora na hata tija yake ni ndogo.

“Tunatoa elimu ya namna ya kuboresha nyanda za malisho na kutumia mbegu bora za malisho, na tutawafundisha wafugaji namna ya kuhifadhi maeneo yao ili sasa wafuge kisasa na wapate tija zaidi,” alisema Mwilawa.

Alisisitiza kuwa sekta ya mifugo ni miongoni mwa sekta zinazoliingizia taifa fedha nyingi za kigeni na hivyo ni lazima juhudi zifanyike za pamoja ili kuiboresha.

Hata hivyo baadhi ya wafugaji waliohudhulia mkutano huo, walisema elimu ya namna ya kufuga kisasa ni muhimu kwao kwa sasa kutokana na kukerwa na migogoro ambayo imekuwa ikiibuka.

Mmoja wa wafugaji hao, Dishon Kalonga, alisema wanahitaji kupatiwa elimu ambayo itawawezesha kuwa na mifugo michache inayoendana na maeneo yao ya malisho.

Habari Kubwa