TAMPA yataja mambo 4 kikwazo sekta ya maziwa

07Dec 2018
Dege Masoli
Tanga
Nipashe
TAMPA yataja mambo 4 kikwazo sekta ya maziwa

CHAMA cha wasindika maziwa nchini (TAMPA), kimeiomba serikali kushughulikia mambo manne yaliyotajwa kuwa ni kizingiti cha kuwekeza katika sekta ya usindikaji maziwa, ikiwamo kodi.

Katibu Mkuu wa TAMPA, Yohana Kubini, aliiambia Nipashe katika mahojiano wakati alipokuwa akizungumzia
mafanikio na changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

Kubini alieleza changamoto hizo kuwa ni tozo ya VAT kwa asilimia 18 iliyorejeshwa na serikali kwenye maziwa na bidhaa zake zilizosindikwa jambo alilolieleza kuwa limekatisha tamaa wawekezaji wengi wa ndani na nje kutokana na ongezeko la gharama za uendeshaji.

Kodi nyingine kwa mujibu wa Kubini ni kodi zinatozwa kwenye umeme, maji, usafirishaji mafuta, vifungashio na vipuli
vinavyotozwa kwa msindikaji na kwa bidhaa za maziwa zilizosindikwa kama mtindi, jibini, siagi ambazo hutozwa ongezeko la thamani (VAT) na yasiyosindikwa, kama maziwa freshi.

"Changamoto nyingine ni uhaba wa vifungashio na gharama kubwa za vifungashio vya maziwa ikichangiwa na uwepo wa kodi ya VAT kwenye vifungashio, ikiwa pamoja na kuwapo na watoa huduma wachache katika sekta ambayo kwa ujumla inaathiri bei za maziwa sokoni," alisema.

Alisema kukua kwa ongezeko la uingizwaji wa bidhaa za maziwa toka nje kwa zaidi ya asilimia tisa kwa mwaka ni changamoto na kwamba utafiti wa masoko uzilizofanyika karibuni zinaonyesha kuwa bidhaa za maziwa toka nje kwa sasa inakadiriwa kumiliki asilimia 48 ya soko la maziwa yaliyosindikwa nchini.

Akizungumzia hali ilivyo sasa ya uwekezaji nchini, alisema baada ya serikali kuondoa kero zinazohusiana na masuala ya kodi kama VAT kwenye vyombo vya kubebea maziwa na mitungi ya kupoza maziwa, ilileta hamasa na kuvutia uwekezaji mkubwa kwa wasindikaji wa maziwa waliopo na wapya ndani ya nchi na nje.

Alisema kufutwa kwa kodi hizo kuliongeza ukusanyaji na usindikaji wa maziwa toka lita 59,515 mwaka 2007 hadi lita 112,500 mwaka 2012 na mwaka 2016 usindikaji ulikuwa lita 155,000 kwa siku sawa na ongezeko la asilimia 20.

Alisema uamuzi huo ulianza kutekelezwa kuanzia mwezi Januari, 2013 na kudumu kwa miaka miwili tu hadi Julai, mwaka 2015 ilipoondolewa wakati sheria mpya ya VAT 2014 ilipoanza kutekelezwa na mpaka kufikia sasa hali haijawa nzuri kwenye sekta hiyo.

Hata hivyo, alieleza malengo ya chama hicho kuwa ni kufikia kiwango cha usindikaji nchini cha lita 400,000 kwa siku ifikapo mwaka 2021 na hivyo kuliingizia taifa zaidi ya Sh. bilioni nane kwa mwaka kama kodi ya mapato na wastani wa ajira zaidi ya 16,000 na kutumia asilimia 100 ya malighafi ya maziwa nchini.

Kubini alieleza kuwa kiwango hicho kinatarajiwa kufikiwa endapo serikali itakubali ombi la kuondoa kodi ambazo ni kero kwenye sekta hiyo na kwamba licha ya baadhi kushughulikiwa, lakini bado kunachangamoto kubwa katika VAT.

Alisema kuondolewa kwa kodi hiyo ni ukombozi kwa mfugaji na mwekezaji, kwa kuwa wastani wa bei ya maziwa ghafi toka kwa mfugaji kwa sasa nchini ni Sh. 700 kwa lita, hivyo kwa usindikaji wa kiwango cha lita 400,000 kwa siku utawafanya wafugaji kupata Sh. milioni 280 kwa siku sawa na Sh. bilioni 100. 8 kwa mwaka.

“Bei ya soko kwa maziwa yaliyosindikwa kwa mlaji ni wastani wa Sh. 2,000 kwa lita ukitoa gharama za usindikaji na manunuzi ya malighafi ya Sh. 1600 kwa lita utaliwezesha taifa kupata kiasi cha Sh. bilioni 8.7 kama kodi ya mapato,” alisema.

Alidai kuwa hali hiyo inabadilisha historia ya Shirika Ia Taifa la Kusindika Maziwa (TDL) lililokuwa na viwanda sita nchini ambalo lilisindika na kufikia kiwango kikubwa cha usindikaji cha wastani wa lita 500,000 kwa siku kwa wakati huo kikitumia asilimia 90 ya maziwa kutoka msaada wa maziwa ya unga toka Benki ya Dunia na kwamba asilimia 10 tu ndiyo iliyotokana na wafugaji wa hapa nchini.

Habari Kubwa