Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Hifadhi wa TANAPA wa Ofisi ya Kiunganishi Dodoma, Dk. Noelia Myonga, alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za taasisi hiyo.
Alisema mikakati mbalimbali ambayo imewekwa na TANAPA, itasaidia kuongeza idadi ya watalii na kuongeza pato la taifa ikiwa ni pamoja na kupitia vivutio mbalimbali vilivyopo nchini.
“Sekta ya utalii nchini kwa hivi sasa inachangia pato la taifa kwa asilimia 17 na inachangia fedha za kigeni kwa asilimia 24,” alisema.
Dk. Myonga alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vingi ambavyo ni muhimu kuvitembelea lakini bado kuna tatizo la Watanzania wengi kutokuwa na mwamko wa kutembelea kwa kisingizio cha gharama kubwa.
Alisema Tanzania ina hifadhi 22 na kila moja ina mvuto wake na maajabu yake ambayo hayapatikani kwingineko duniani.
“Gharama si kisingizio kwani kwa watalii wa ndani kwa kuwa serikali imewapendelea wazawa ambao wanapenda kutembelea hifadhi zetu kwa kuweka gharama ya Sh. 11,800 kwa hifadhi kubwa na zile zingine ni Sh. 5,000 kiasi ambacho mtanzania anaweza kukimudu,” alisema.
Alizitaja hifadhi hizo kuwa ni Arusha, Burigi -Chato, Gombe, Ibanda -Kyerwa, Katavi, Kigosi, Kilimanjaro, Kisiwa cha Rubondo, Kisiwa cha Saanane, Kitulo, Manyara, Mikumi, Mhale, Udzungwa, Mkomazi, Mto Ugala, Nyerere, Ruhaha, Rumanyika Karagwe, Saadani, Serengeti na Tarangire.
"Kila hifadhi imekuwa na mvuto wake tofauti kabisa. Mfano Hifadhi ya Manyara kuna Simba ambao wanapanda miti na ndege wazuri na waajabu na hifadhi ya Tarangire kuna tembo wengi na mibuyu mikubwa ambayo inavutia zaidi. Hifadhi ya Saadani kuna kasa wakubwa na wa kijani na vivutio vingi katika hifadhi mbalimbali," alisema Dk. Myonga.
Pamoja na kuhamasisha watu kutembelea hifadhi za taifa, alisema kuna haja ya Watanzania kujenga tabia ya kutembelea maeneo ya kihistoria ikiwamo michoro ya Kondoa Irangi, Kongwa maeneo ya wapigania uhuru.