TANESCO yataja kiini umeme kukatika

13Jan 2021
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
TANESCO yataja kiini umeme kukatika

SHIRIKA la Umeme (TANESCO) Mkoa wa Dodoma, limesema kukatika kwa umeme mara kwa mara kwenye baadhi ya maeneo kumetokana na wananchi kuchoma nguzo za umeme wakati wa kiangazi.

Kutokana na kikwazo hicho, shirika hilo limewataka wananchi kuhakikisha wanapochoma nyasi, wazingatie umbali wa hatua 10 kutoka kwenye nguzo.

Meneja wa TANESCO mkoani hapa, Frank Chambua, aliyasema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini hapa.

Alisema baadhi ya wananchi wakati wa kiangazi wamekuwa wakichoma nyasi karibu na nguzo za umeme, jambo linalochangia nguzo nyingi kupata hitilafu na kuliwa na mchwa.

“Unakuta nguzo zaidi ya 40 kwa siku zimedondoka chini katika maeneo mbalimbali, suala hilo linachangia tatizo la umeme kukatika katika eneo, husika kwa sababu tayari kunakuwa na uharibifu wa miundombinu hiyo,” alisema.

Alisema TANESCO itaendelea kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha wanajua umuhimu wa kutoharibu miundombinu hiyo, ili wasisababishe hitilafu za umeme.

Aliwataka wananchi walio pembezoni kuhakikisha kila mmoja anakuwa mlinzi wa mwenzake ikiwamo kutoa taarifa pale wanapoona kuna uharibifu wa miundombinu inayojengwa na shirika kwa ajili ya kusambaza umeme.

Akizungumzia shida ya njia ya Mpwapwa kukatika umeme mara kwa mara, meneja huyo alisema inatumia kituo cha kupoza umeme cha Zuzu, hivyo kila kunapohitajika kufanya matengenezo, lazima umeme ukatwe kwa muda.

"Kituo cha NARCO Kongwa kikikamilika na kuanza kufanya kazi, kitasaidia kupunguza tatizo la kukatika umeme mara kwa mara katika njia hiyo," alisema Chambua...soma zaidi kupitia https://epaper.ippmedia.com

Habari Kubwa