TANESCO yatoa angalizo uharibifu wa miundombinu

23Feb 2021
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
TANESCO yatoa angalizo uharibifu wa miundombinu

KUTOKONA na maji kuendelea kuingia kwa mita za ujazo kati ya 600 hadi 1,000 kwa sekunde katika mabwawa ya kufua umeme ya Mtera na Kidatu, Shirika la Umeme (TANESCO) limewata wakazi wa maeneo hayo wanaoendesha shughuli za kijamii kuchukua tahadhari ili kuepuka uharibifu wa miundombinu.

Baadhi ya wakazi wanaoishi pembezoni mwa mkondo wa maji yatokayo katika mabwawa ya kufua umeme ya Mtera na Kidatu, wamekuwa wakifanya shughuli za kilimo na ufugaji katika maeneo hayo jambo ambalo ni hatari hususani kipindi hiki cha mvua zinazoendekea kunyesha.

Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Meneja wa kituo cha kufua umeme Mtera, Mhandisi Elias Mwalupilo, alipotembelea eneo hilo na kubaini maji kuendelea kuingia katika mkondo huo.

"Kutokana na kina cha maji kinazidi kuongezeka, itatulazimu hapo baadaye kama hali itaendelea kuwa hivi kupunguza maji yaliyozidi kwa kuruhusu kupita kwenye mkondo wake wa asili kwa ajili ya usalama wa miundombinu ya umeme pamoja na daraja," alisema Mhandisi Mwalupilo.

Alisema Shirika linalazimika kuyapunguza maji yaliyozidi kina cha juu cha bwawa ambacho ni 698.50 kwa ajili ya usalama wa bwawa na mitambo ya kufua umeme ili iendelee kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Mhandisi Mwalupilo, alisema kutokana na mvua nyingi ambazo zilinyesha mwaka jana hasa Nyanda za Juu Kusini Mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe ambako, kuna vyanzo vingi vya maji ilipelekea bwawa la Mtera kupata maji mengi, hivyo uwepo wa mvua za wastani mwaka huu kumepelekea kina cha maji katika bwawa la Mtera kuongezeka.

Mhandisi Mwalupilo alivitaja vijiji vinavyotakiwa kuchukua tahadhari kwa upande wa mkondo wa Mtera ni Keseke, Idodoma wilayani Mpwapwa, kwa Kilolo ni Nyanzwa na Ruaha Mbuyuni, Wilaya ya Kilosa ni Malolo, Msosa na Kidai ‘A’ na ‘B’.

Mhandisi huyo alisema vijiji vinavyotakiwa kuchukua tahadhari kwa upande wa bwawa la Kidatu Wilaya ya Kilosa ni Vidunda, Ruaha, Lyahira na Kitete na Vijiji vilivyopo Kilombero ambavyo ni Nyange, Msolwa station na viwanda vya sukari Kilombero.

Naye Meneja Uhusiano TANESCO, Johary Kachwamba, ametoa wito kwa wananchi hao wa pembezoni kuchukua tahadhari ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea wakati wa zoezi la kuyaruhusu maji kupita kwenye mkondo wake wa asili.

Alisema TANESCO itaendelea kutoa elimu kwa wananchi hao, lakini pia kushirikiana na viongozi wa vijiji, Mamlaka ya Bonde la Mto Rufiji pamoja na maofisa wa uvuvi kwa kuzingatia jamii kubwa katika vijiji hivyo inayojishughulisha na kilimo, ufugaji na uvuvi.

Habari Kubwa