Tani 1,700 za mbaazi zakosa soko

28Sep 2020
Said Hamdani
Lindi
Nipashe
Tani 1,700 za mbaazi zakosa soko

TANI 1,700 zao la mbaazi mkoani Lindi zimekaa kwenye maghala kutokana na kukosa wanunuzi, jambo ambalo limewaweka wakulima njiapanda.

Mbaazi hizo ni za wilaya za Nachingwea na Ruangwa na zimehifadhiwa kwenye maghala yanayomilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika ununuzi wa mazao  (RUNALI).

Mrajisi wa vyama vya ushirika mkoani Lindi, Edmund Massawe, aliyasema hayo wakati akijibu maswali na malalamiko yaliyowasilishwa na wajumbe kwenye kikao cha tathmini ya zao hilo kilichofanyika mjini humo.

Alisema kukosekana kwa wanunuzi tani 1,700 za zao la mbaazi kati yake 540 zipo maghala ya wilayani Ruangwa.

Massawe alisema wapo baadhi ya wanunuzi walijitokeza kutaka kununua mbaazi hizo kwa bei ya Sh. 400 kwa kilo kwa masharti ya kutolipa aina yeyote ya ushuru ukiwamo ule wa Serikali za Mitaa jambo ambalo kimsingi limekuwa gumu kukubalika.

“Kuna wanunuzi walijitokeza kutaka kuzinunua mbaazi hizo, lakini wakatoa masharti eti wasilipe aina yeyote ya ushuru wa serikali na kijiji,’’ alisema Massawe bila kutaja majina ya wanunuzi hao.

Awali, wakiwasilisha madai au malalamiko hayo kwa Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Hashimu Komba, alitaka kufahamu hatima ya wakulima wenye tani 1,700 za mbaazi katika maghala mbalimbali ndani ya wilaya hizo.

Habari Kubwa