Tanzania, Afrika Kusini zaunda kamati ya kuratibu ushirikiano

26Sep 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Tanzania, Afrika Kusini zaunda kamati ya kuratibu ushirikiano

TANZANIA na Afrika Kusini zimeunda kamati ya pamoja yenye wajumbe kutoka nchi hizo ili kushirikiana katika kutekeleza hati ya makubaliano (MoU) kwenye masuala ya viwanda, biashara na uwekezaji.

Hatua hiyo ilifikiwa jana jijini hapa katika kikao cha pamoja kati ya Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Ally Gugu, na ujumbe kutoka Ubalozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania.

Akizungumza na ujumbe huo, Gugu alisema nchi hizo zimekuwa na ushirikiano wa kibiashara, kiuchumi na kisiasa kwa muda mrefu tangu kipindi cha kudai uhuru.

“Hivyo ni jambo jema kushirikiana katika kuendeleza biashara kati ya nchi hizi mbili, na ushirikiano huu umezidi kuimarika kwa uwapo wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). Nchi hizi mbili zilikubaliana kuwa na hati ya makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya viwanda na biashara,” alisema.

Alisema lengo la hati hiyo ni kuimarisha uhusiano wa kibiashara zaidi kwa kuongeza biashara kwa maslahi ya pande zote mbili hasa ikizingatiwa Afrika Kusini ni moja ya nchi vinara katika uwekezaji barani Afrika.

Naye Kaimu Balozi wa Afrika Kusini nchini, Sizwe Mayoli, alisema amefurahi kupata fursa ya kujadili masuala ya ushirikiano wa kiuchumi, kibiashara na uwekezaji baina ya Tanzania na nchi yake katika kikao hicho.

Alisema baadhi ya masuala yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na kupata taarifa ya hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa hati hiyo ya ushirikiano katika sekta ya viwanda, biashara na uwekezaji.

“MoU hii inatoa fursa ya kuunda kamati ya pamoja ya biashara na uwekezaji katika nchi hizi mbili, hivyo kikao chetu kimehitimishwa kwa kuunda kamati hii ili kushirikiana pamoja katika kutekeleza hati ya makubaliano,” alisema.

Habari Kubwa