Tanzania, DRC kufanya kongamano la kibiashara

19Sep 2016
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Tanzania, DRC kufanya kongamano la kibiashara

KONGAMANO la kibiashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), linatarajiwa kufanyika Septemba 22, mwaka huu jijini Lubumbashi.

Bw. Godfrey Simbeye.

Lengo la kongamano hilo ni kukuza mazingira ya uwekezaji, viwanda, usafirishaji na biashara.

Washiriki wa kongamano hilo ni Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo nchini (TCCIA) na kampuni ya 361 Degrees.

Ofisa Biashara wa Tantrade, Getrude Ngweshen, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kuwa nchi hizo mbili zimeshirikiana kufanya kongamano ili kutoa fursa za uwekezaji katika ukanda wa uchumi wa Tanzania na DRC.

Alisema DRC ilionyesha nia yake ya utafutaji nishati na madini kwa Tanzania baada ya mkutano wa mashauriano uliofanyika Agosti, mwaka huu na hivyo kupendekeza Jiji la Kinshasa kupokea mafuta kupitia bomba la mafuta kutoka Bandari ya Tanga hadi Hoima nchini Uganda.

Alisema kongamano hilo litakusanya wafanyabiashara zaidi ya 100 kutoka sekta binafsi za Tanzania na DRC na kuwahusisha watoa maamuzi na sera wa serikali kutoka nchi hizo mbili.