Tanzania yafikia pazuri kwa matumizi ya fedha kidijitali

22Sep 2016
Amri Lugungulo
Nipashe
Tanzania yafikia pazuri kwa matumizi ya fedha kidijitali

UTAFITI uliofanywa na Umoja wa Mataifa kupitia taasisi ya Better Than Cash Alliance, umeonyesha Tanzania imepiga hatua nzuri ya matumizi ya mfumo wa malipo ya fedha kwa kutumia dijitali.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi Mtendaji wa Better Cash Alliance, Dk. Ruth Goodwin, jijini Dar es Salaam jana ilieleza kuwa Tanzania imepata uzoefu mkubwa ambao umechangia ongezeko la mapato.

Alisema mfumo huo umesaidia kuongeza faida kwa wananchi wanaotumia mfumo huo na upo uwezekano wa Tanzania kujenga misingi imara ya ukuaji wa uchumi kupitia mfumo huo.

Dk. Godwin alisema utafiti huo umebaini siri ya mafanikio ya serikali yoyote yanayotokana na wananchi wake pamoja na wafanyabiashara kutumia mfumo wa malipo wa dijitali.

''Nchi mbalimbali ambazo uchumi unachipukia, hutegemea namna zinavyoboresha mfumo wake wa uchumi hasa unapokuwa na uwazi, ushirikishwaji wa kifedha na katika utafiti huu umeonyesha kuwa mfumo wa malipo ya digitali unaofanywa na serikali ya Tanzania hivi sasa, umepata mafanikio makubwa,“ alisema Dk. Godwin.

Alisema kuwa kutokana na Serikali ya Tanzania kutumia mfumo wa malipo wa dijitali, imefanikiwa kuimarisha sekta ya utalii kwa kupunguza mianya ya kupoteza mapato kupitia malipo ya fedha taslimu hususan malipo ya kuingia mbuga za wanyama kwa zaidi ya asilimia 40 na kusaidia uwekezaji na ajira.

Mfumo huo wa kisasa pia lisema umesaidia kupunguza urasimu ikiwa ni pamoja na kupunguza muda wa forodha kutoka siku tisa hadi chini ya siku moja na umeongeza uwazi kati ya raia na serikali.

Aliongeza kuwa kwa kutumia mfumo wa malipo ya kodi ya dijitali, mfumo huo umesaidia kuhakiki malipo kielektroniki na kuzuia undanganyifu.

Aidha, Dk. Godwin alisema utafiti huo pia unaonyesha maeneo muhimu ambayo nchi inaweza kukuza maendeleo ya uchumi kwa haraka ni kupitia malipo ya kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa mfumo wa dijitali na urasimishaji wa biashara.