Tanzania yapiga hatua kilimo cha mbogamboga

01Aug 2020
Renatha Msungu
Arusha
Nipashe
Tanzania yapiga hatua kilimo cha mbogamboga

TANZANIA imepiga hatua katika kilimo cha mbogamboga baada ya kufanikiwa kuongeza aina 19 za mbegu za mbogamboga na viungo, watafiti wamebaini.

Wataalamu hao pia wamesema Tanzania iko mbioni kuikamata Kenya katika uzalishaji wa bidhaa hiyo, wakibainisha kuwa takwimu za sasa zinaonyesha Tanzania inapata Sh. milioni 800 kwa mwaka wakati Kenya wanakusanya Sh. bilion moja kutokana na kilimo hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Kituo cha Utafiti wa Mbegu za Mbogamboga, Dk. Gabriel Rugalema, alisema mbegu hizo zimeonyesha kuwa na soko kubwa duniani.

Alisema aina hizo za mbegu zinaoteshwa katika vitalu kwenye bustani yao na zinauuzwa kwa wakulima mbalimbali nchini na nje ya nchi.

Dk. Rugalema pia alisema wamekuwa wakitoa mafunzo kwa wakulima wanaopata mbegu, akibainisha kuwa wateja wao hao wamegawanyika katika makundi matatu, likiwamo la wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali nchini.

Alibainisha kuwa wakulima hao ni kutoka mikoa ya Mtwara, Manyara, Kilimanjaro, Moshi, Arusha na Zanzibar.

Dk. Rugalema alisema kituo cha uzalishaji mboga cha jijini Arusha kina fursa ya kufundisha vikundi namna ya utunzaji mbegu ili kuwapa manufaa katika kilimo wanachofanya.

"Tumekuwa tukifundisha watu ili kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa, tunafanya jitihada za kuinua kilimo cha mbogamboga na viungo," alisema Dk. Rugalema.

Aliishukuru serikali kwa kuwaongeza mkataba wa kuendelea kuwa nao, akiahidi kupanua zaidi huduma zao.

Mkulima Gilbert Mushi alisema kituo hicho kimekuwa msaada mkubwa kwao kutokana na kuwapa elimu kuhusiana na kilimo cha mbogamboga.

"Tunakishukuru kituo hiki kwa kututoa kwenye kilimo cha hasara na kutuingiza kilimo cha faida, tunaona matunda yake, " alipongeza mkulima huyo.

Habari Kubwa