TARI kugawa bure mbegu Nanenane

01Aug 2020
Grace Mwakalinga
Mbeya
Nipashe
TARI kugawa bure mbegu Nanenane

TAASISI ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Kituo cha Uyole, inakusudia kutoa bure mbegu za mazao ya aina mbalimbali kwa wakulima watakaotembelea banda lake kwenye viwanja vya maonyesho ya kilimo maarufu Nanenane, jijini Mbeya, ili kuwajengea wananchi utamaduni wa kutumia mbegu za kisasa.

Mratibu wa utafiti wa zao la viazi mviringo kitaifa ambaye pia ni Mtafiti Mkuu wa Kilimo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), Kituo cha Uyole, Dk. Juma Kayeke, akiwaonyesha waandishi wa habari, kituoni hapo, jijini Mbeya jana, mbegu za viazi ambazo zitatumika katika maonesho ya Nane Nane, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, ambayo yatafanyika kwenye Viwanja vya John Mwakangale Mbeya. PICHA: GRACE MWAKALINGA

Ofisa Ughani wa taasisi hiyo Kituo cha Uyole, Nyimila Kalindile, alitangaza neema hiyo kwa wakulima alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mwisho ya banda la maonyesho la taasisi hiyo.

Alisema wameamua kufanya kwa lengo la kuhamasisha wakulima kutembelea taasisi hiyo na kujifunza teknolojia na elimu ya kilimo bora.

“Mwaka huu katika maonyesho ya Nanenane tunatoa ofa kwa wakulima ambao watatembelea banda letu la TARI Uyole kupewa mbegu za maharage ili kwenda kufanya majaribio na kuona ubora wake,” alisema Kalindile.

Mkurugenzi wa TARI Kituo cha Uyole, Dk. Tulole Bucheyeki, alisema taasisi hiyo imeongeza idadi za mbegu mpya za mazao ya aina mbalimbali ambazo zitaonyeshwa kwa wananchi kwa mara ya kwanza wakati wa maonyesho ya kilimo ya mwaka huu ambayo yanaanza leo kwenye Viwanja vya John Mwakangale jijini.

Alisema mbegu hizo ambazo zimebuniwa na kituo hicho, zina ubora na zitaongeza uzalishaji kwa mkulima, hivyo akawahamasisha kujitokeza kwa wingi kujifunza maarifa na teknolojia mpya.

Baadhi ya watafiti walisema mbali na uwepo wa mbegu mpya za mazao, pia wameandaa teknolojia mpya na za kisasa ambazo kumwezesha mkulima mdogo kuachana na kilimo cha mazoea na kuanza kulima kisasa.

Habari Kubwa