TARI kutoa elimu kilimo maonyesho Nanenane

24Jun 2022
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
TARI kutoa elimu kilimo maonyesho Nanenane

TAASISI ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) imeanza maandalizi ya teknolojia, mbegu, zana na mbinu bora za kilimo kwa ajili ya kufundishia wakulima kwenye Maonyesho ya Wakulima, maarufu Nanenane, ambayo kitaifa yatafanyika jijini Mbeya.

Timu ya watafiti wa taasisi hiyo kutoka Makao Makuu imeungana na wenzao wa Kituo cha Uyole kilichoko jijini Mbeya kuandaa teknolojia hizo katika viwanja vya John Mwakangale yatakakofanyikia maonyesho hayo kitaifa.

Watafiti hao wameanza maandalizi hayo kutokana na maelekezo ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ambaye aliwataka kuhakikisha teknolojia za kisasa zinaandaliwa kwenye maonyesho hayo ili wakulima wajifunze na wakazitumie kwenye uzalishaji wa mazao.

Mkurugenzi wa Uhawilishaji wa Teknolojia kutoka TARI, Juliana Mwakasendo, alisema jana kuwa baada ya kupokea maelekezo ya waziri, waliamua kupiga kambi katika Uwanja wa John Mwakangale kwa ajili ya kushughulikia vipando mbalimbali ambavyo vimeandaliwa.

Alisema kwenye maonyesho hayo, watafiti kutoka katika vituo vyote 14 vya TARI nchini watakuwapo kwa ajili ya kuhakikisha wakulima wanafundishwa mbinu bora za kilimo cha mazao kuanzia hatua za awali mpaka kwenye uhifadhi.

“Kwa hiyo, tunawashauri wakulima wote nchini kuhakikisha wanatembelea kituo chetu ili kupata mbinu za kisasa za uzalishaji wa mazao mbalimbali, wataalamu wa mazao tofauti watakuwapo hapa na watakuwa wanawafundisha wakulima,” alisema Mwakasendo.

Meneje Usambazaji wa Teknolojia na Biashara wa TARI, Magreth Mchomvu, alisema taasisi hiyo ilianza kuandaa teknolojia na vipando tangu mwezi Februari mwaka huu baada ya kupata taarifa za awali kwamba mwaka huu kutakuwa na maonyesho.

Alisema walianza kwa kuandaa vipando vya mazao ambayo yanachukua muda mrefu kukomaa ili kuendana na muda wa maonyesho na mpaka sasa baadhi ya mazao hayo yameanza kukomaa na wana matumaini kwamba mpaka kufikia Agosti Mosi yatakuwa yamekomaa.

Aliwataka wakulima wa maeneo mbalimbali kuhakikisha wanatembelea maeneo hayo wakati wa maonyesho ili wajifunze mbinu za kisasa ambazo zitawasaidia kuzalisha kwa tija tofauti na walivyozoea.

“Tunamshukuru Mheshimiwa Waziri Bashe kwa kuyaleta maonyesho haya Mbeya kwa sababu tuna imani kwamba ukanda huu ni muhimu sana kwa uzalishaji wa mazao kitaifa na hili ndilo ghala kuu la chakula kwa nchi yetu,” alisema Magreth.

Mkurugenzi wa TARI Kituo cha Uyole, Dk. Tulole Bucheyeki, alisema kuwa kutokana na maonyesho hayo kufanyika kitaifa Mbeya, wamefanya maandalizi makubwa tofauti na walivyokuwa wanaandaa miaka mingine na kwamba watahakikisha yanakuwa na mafanikio.

Alisema wameandaa vipando vya mazao mbalimbali na kwa kutumia teknolojia tofauti ili kuwaelekeza wakulima wakati wa maonyesho na baada ya maonyesho.

Alisema miaka ya nyuma walikuwa wanaandaa maonyesho hayo kwa ajili ya wakulima wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini pekee lakini mwaka huu wameandaa kwa ajili ya nchi nzima na ndiyo maana wataalamu wa vituo vyote 14 watakuwapo.

“Teknolojia za kanda zote zitakuwapo hapa maana wataalamu wote watakuwapo hapa, wakulima wakija hapa watajifunza mbinu zote muhimu za kilimo,” alisema Dk. Bucheyeki.

Mtafiti wa Afya ya Udongo kutoka kituo cha TARI Kifyulilo cha Mafinga mkoani Iringa, Emmanuel Kadogolo, alisema wakulima pia watafundishwa namna ya kupima afya ya udongo na namna ya kurejesha rutuba kwenye mashamba yao.

Habari Kubwa