TARI yakunwa utekelezaji agizo la JPM

21Nov 2020
Ashton Balaigwa
Singida
Nipashe
TARI yakunwa utekelezaji agizo la JPM

WAJUMBE wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), wameridhishwa na utekelezaji wa majukumu ya watafiti na watendaji yaliyotolewa na Rais John Magufuli, katika uendelezaji wa zao la korosho nchini.

Mwenyekiti wa Bodi ya TARI, Dk.Yohana Budeba, aliyasema hayo baada ya kutembelea mashamba mapya ya korosho katika Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.

Dk. Budeba alisema maagizo ya serikali yaliyotolewa ya kupanua kilimo cha korosho kwenye mikoa mipya, utekelezaji wake umeshaanza kwa kasi kwenye mikoa ambayo ilikuwa hailimi zao hilo.

Alisema utekelezaji huo umeshaanza kwenye mikoa ya Dodoma, Morogoro, Iringa, Singida, Tabora, Katavi, Songwe, Kigoma , Kilimanjaro, Mbeya, Njombe na Ruvuma, kwamba tayari wananchi wamepewa elimu ya zao hilo, pamoja na kuanzisha vitalu vya uzalishaji wa miche ya korosho.

“Sisi kama bodi tumeridhishwa sana na watafiti namna walivyotekeleza agizo la Rais Magufuli katika kuinua kilimo cha korosho kwenye mikoa mipya,” alisema Dk. Budeba.

Mmoja wa wajumbe wa bodi hiyo, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Vikundi Vidogo vya Wakulima Tanzania (Mviwata), Stephen Ruvuga, alisema utekelezaji wa agizo Rais Magufuli utaifanya nchi kuinuka kiuchumi.

Mjumbe mwingine wa bodi hiyo, Dk. Erick Shirima, alitaka watafiti hao kuendelea kuzalisha kwa wingi mbegu za korosho, kutokana na wakulima wengi kuitikia wito wa kulima zao hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk. Geofrey Mkamilo, alisema katika kutekeleza maagizo ya Rais Magufuli, wameweka mkakati wa kuongeza uzalishaji wa korosho kutoka tani 315,000 za sasa, hadi tani milioni moja ifkapo mwaka 2023.

Mwenyekiti wa wakulima wa korosho katika Wilaya ya Manyoni, Issa Madenge, alishukuru serikali kwa kuamua kuendeleza zao hilo kwa mikoa ambayo haikuwa inalima korosho, akisema itasaidia kuwainua kiuchumi wakulima.

Habari Kubwa