Tasaf yatoa mizinga 116 kwa kaya maskini

21Jan 2019
Anceth Nyahore
 LONGIDO
Nipashe
Tasaf yatoa mizinga 116 kwa kaya maskini

MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), wilayani Longido, umekabidhi mizinga 116 yenye thamani ya Sh. milioni 26 kwa kaya 75 maskini katika Kijiji cha Kitendeni, Tarafa ya Enduimet, kwa ajili ya ufugaji wa nyuki.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Longido, Toba Nguvila (aliyevaa shati la mistari), akigawa mizinga 116 ya kufugia nyuki kwa kaya maskini 75 za Kijiji cha Kitendeni, zinazonufaika kupitia mpango wa Tasaf wa kuwainua wananchi wenye hali ngumu kiuchumi. PICHA: ZANURA MOLLEL

Akikabidhi mizinga hiyo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Longido, Toba Nguvila, alisema kipaumbele cha kwanza kwa serikali ni kuwainua wananchi wenye hali ngumu ya kimaisha.

Alisema serikali kupitia Tasaf inashughulika na watu hao wanaotoka kwenye kaya duni.

"Pongezi kwa Tasaf Longido kwa kuwajali watu hawa, mnatekeleza agizo la serikali ipasavyo," alisema.

Alisema awali hali za wanufaika hawa kabla hawajaingia kwenye mradi ilikuwa mbaya, lakini kupitia ruzuku hizo wajikwamue kiuchumi kabla ya mpango huo kufikia mwisho.

"Wanufaika ni wengi mno naomba kubalini kubadilisha maisha yenu kupitia ruzuku hizi mnazopewa, msiende kunywea pombe wala kuongeza mke," alisema.

Alisema wataelekezwa namna ya kuitumia mizinga hiyo ili kuzalisha asali bora ambayo itawaongezea kipato kwa kuiuza katika masoko makubwa.

Hata hivyo, alimtaka mtaalamu wa nyuki kutoka halmashauri, kuwatembelea mara kwa mara wanufaika wa mizinga hiyo na kuwapa elimu.

Alisema endapo mizinga hiyo itashindwa kuzalisha kama inavyotarajiwa, atachukuliwa hatua za kinidhamu.

Alimtaka Ofisa Ushirika wa Halmashauri kushirikiana na vikundi hivyo kuwafundisha na kuwaelimisha namna ya kuibua fursa za kiuchumi waweze kuinuka na kupiga hatua katika kipato chao.

Aidha, alimtaka Ofisa Biashara kuhakikisha anatafuta soko la kudumu ndani na nje ya nchi, ili watakapofikia kurina asali, wasibabaike kupata soko.

Kwa upande wake, Mratibu wa Tasaf Wilaya ya Longido, Saruni Lobulu, alisema mizinga hiyo imekabidhiwa kwa vikundi vitano kati ya saba vilivyopo katika kijiji hicho ambavyo vipo kwenye mpango wa Tasaf.

Akifafanua alisema mizinga hiyo ina thamani ya Sh. milioni 26 na itagawanywa kwa watu 75 na kila kikundi kitapewa mizinga 15.

"Watu hawa wamegawanywa kwa vikundi vya watu 15, na tutatoa mizinga 15 kwa kila kikundi," alisema.

Alieleza watatoa mafunzo ya ufugaji nyuki kwa walengwa hao na wanatarajia kuanza ujenzi wa barabara waliyoibua walengwa ya kilomita 4.5 pindi fedha zitakapopatikana.

"Tunatengeneza miradi mingi na hii wanaibua walengwa wenyewe," alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Juma Mhina, aliishukuru Tasaf kwa kuendelea kuchangia miradi ya maendeleo ikiwamo ufugaji wa nyuki na kwamba kupitia ufugaji nyuki unaotekelezwa na wakazi wa Kijiji cha Kitendeni, anaamini walengwa hao watajikwamua kiuchumi.

"Lakini kubwa zaidi niseme tu utafiti umefanyika na kugundulika misitu ya Longido inazalisha asali nzuri duniani kote na asali hii haina sumu kwa kuwa huzalishwa na maua ya aina moja.

"Longido kuna miti aina ya acacia (oltepes), miti hii ni mizuri katika uzalishaji wa asali dunia nzima na inapatikana Longido," alisema.

Aliwataka wakazi wa Longido kujitokeza na kuwekeza katika miradi ya ufugaji nyuki, kwa kuwa maeneo mengi wilayani hapo yanafaa kuwekeza katika miradi ya nyuki, misitu ipo ya kutosha.

Mmoja wa wanufaika wa mizinga hiyo, Anna Elisha, alisema Tasaf imemsaidia kuwasomesha watoto wake pamoja na kuhakikisha wanapata milo mitatu kwa siku na kukata bima ya afya.

Habari Kubwa