Tasaf yamwezesha kijana kuanzisha kiwanda kidogo

20Nov 2019
Elizaberth Zaya
Njombe
Nipashe
Tasaf yamwezesha kijana kuanzisha kiwanda kidogo

AWARD Juma, mkazi wa Mtaa wa Ramadbania mkoani Njombe, amekuwa kivutio kwa wananchi wa mkoa huo, baada kuanzisha kiwanda kidogo cha kutengeneza viatu ndani ya nyumba yake.

Kijana huyo amefungua kiwanda hicho baada ya kujiwekea akiba kidogo kidogo baada ya kuingizwa katika mpango wa kunusuru kaya masikini tangu mwaka 2015, unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).

Akizungumza mbele ya maofisa wa Tasaf waliomtembelea, Juma alisema kabla ya kuingizwa katika mpango huo, alikuwa anaishi katika mazingira magumu, huku akilea wadogo zake wawili ambao alikuwa ameachiwa na wazazi wake ambao wamefariki.

Alisema kazi pekee ambayo ilikuwa inamsaidia kupata kipato ni kuwashonea watu viatu vinavyokatika, ambayo hata hivyo ilikuwa ya kusuasua kutokana na kutokuwa na wateja.

"Mimi sikufanikiwa kwenda shule kutokana na hali ya maisha kutoka kwa wazazi wangu, kwa hiyo nilikuwa naenda kukaa kijiweni kwa mafundi wanaoshona viatu, na kupitia kwao nilianza kujifunza kidogo kidogo mpaka nikaanza kuwashonea watu,"

Aliongeza: "Nilianza kupata pesa kidogo kutokana na kazi hii, japokuwa ilikuwa haitoshi kwa sababu kwa siku nilikuwa na uwezo wa kupata hata Sh.1, 000 mpaka 1,500, lakini niliwapunguzia wazazi wangu mzigo."

Juma alisema baada ya wazazi wake kufariki na kuachwa wadogo zake wawili ndipo maisha yalizidi kuwa magumu na hata chakula chao cha kila siku kuwa kigumu.

"Tulipata shida sana na hawa wadogo zangu, ila Mungu ni mkubwa mwaka 2015 Tasaf kupitia wananchi wa mtaa huu walituona, wakatuingiza kwenye mpango, wakawa wanatupatia Sh.40000 pesa ambayo naweza kusema kwamba huo ndio ulikuwa mkombozi wangu,"alisema Juma na kuongeza:

"Kwa mara ya kwanza nilihakikisha kwamba naitumia pesa hiyo kwa malengo, kwanza kununulia sare za wadogo zangu shuleni, chakula nyumbani na naweka akiba kwa ajili ya kuboresha kibanda changu cha kushona viatu, kila nilipokuwa nikipewa pesa hiyo nilikuwa naweka akiba kidogo kwa ajili ya 'shoe shine'."

Juma anasema ili kuboresha ushonaji wake, mwaka 2017 alianza kwenda kujifunza kwa wamasai namna wanavyotengeneza viatu vyao na kwamba baada yao hapo akaanza kutengeneza mwenyewe.

"Kama mnavyoona hivi ni viatu ambavyo ninatengeneza mwenyewe, niliamua kutumia nyumba hii niliyoachiwa na wazazi wangu, kwa hiyo hiki ndiyo kama kiwanda changu kwa sasa, na watu wengi wanakuja kunishangaa namna ninavyofanya kazi hii wakati hata sijaisomea, naishukuru sana Tasaf kwa hapa iliponifikisha, lengo langu ni kufungua kiwanda kikubwa niajiri na vijana wengine," alisema Juma

Alisema kwa sasa changamoto kubwa aliyonayo ni ukosefu wa soko na kuiomba serikali kumsaidia kumuunganisha na fursa za masoko.

Mratibu wa Miradi ya Tasaf Mkoa wa Njombe, Peter Magema, alisema tayari wako kwenye mchakato wa kumuunganisha na fursa za masoko.

Habari Kubwa