Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Exaudi Kigahe, aliyasema hayo jana jijini hapa kwenye hafla ya kupokea cheti hicho kutoka Huduma za Ithibati za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADCAS).
Alisema ithibati ina manufaa makubwa kwa taasisi za umma na binafsi na TBS inatoa huduma kwa gharama nafuu kulinganishwa na gharama zinazotozwa na kampuni za nje ambazo zimekuwa zikitoa huduma hizo.
“Hivi karibuni, kampuni ya nje yamepata changamoto kutokana na janga la UVIKO-19 na hivyo kushindwa kutoa huduma kwa wateja wao, hali iliyosababisha wateja wao kupoteza uhalali wa kuwa na vyeti vya uthibitisho wa mifumo ya kimenejimenti,” alisema.
Naibu waziri huyo alisema kutokana na tatizo hilo, baadhi ya taasisi tayari zimefanya uhamisho wa kupata huduma ya uthibitisho wa mifumo ya kimenejimenti kutoka kampuni za nje kwenda TBS ili kunufaika na huduma ya uhakika kwa gharama nafuu.
“Niwapongeze TBS kwa kufikia hatua hii kubwa ya kupata ithibati ya umahiri katika kutoa huduma ya ithibati ya umahiri katika kutoa huduma hii, sina shaka mtaendelea kudumisha na kuongeza wigo kwenye kutoa huduma zenye ithibati ya umahiri ili kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa taifa,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa SADCAS, Victor Mundembe, aliitaka TBS kuhakikisha inazingatia ubora kwenye utoaji huduma hizo ili viwango vya ithibati hiyo visishuke.
“Kama tutabaini viwango vinashuka, tutawanyang’anya hii ithibati,” mkurugenzi huyo alitoa angalizo.
Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora TBS, Lazaro Msasalaga, alitaja hatua mbalimbali za kupata cheti hicho kuwa ni pamoja na kuweka na kufuata mifumo kulingana na matakwa yaliyoainishwa kwenye kiwango cha kimataifa ISO/IEC 17021.
“Kujipima utendaji kwa mujibu wa kiwango husika pamoja na matakwa ya tume ya ithibati na kuwa na wataalamu wenye umahiri na weledi katika dhana nzima ya utoaji huduma,” alifafanua.