TCRA yakumbushwa kampeni yake

14Sep 2017
Mary Geofrey
Nipashe
TCRA yakumbushwa kampeni yake

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeshauriwa  kuendeleza kampeni yake ya kuelimisha umma kuhusu matumizi ya mitandao ijulikanayo kama ‘Futa-delete-kabisa’ ili kusaidia jamii kuondokana na matumizi mabaya ya mitandao.

Aidha, imetakiwa kubuni mbinu na mikakati mipya ya kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao ambayo yanachangiwa na ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano nchini.

Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Kampuni ya Jamii Media Limited (Jamii Forum), Maxence Melo, alitoa rai hiyo jana katika mkutano kati ya Kamati ya Maudhui ya TCRA na mamiliki wa mitandao ya kijamii jijini Dar es Salaam, uliokuwa na lengo la kukumbushana wajibu katika kuhabarisha Watanzania.

“Sijui kwa nini ile kampeni mlioianzisha ya ‘Futa-delete-kabisa’ mliisitisha kwa sababu kwa kiasi kikubwa ilikuwa ikielimisha jamii kuepuka matumizi mabaya ya mitandao na ilisaidia kudhibiti vitendo vya uhalifu, sasa ni wakati wa kuirudisha tena,” alisema.

“Wakati huu, tunadhibiti mitandao ya kijamii kukiuka maadili ya uandishi wa habari na kuzingatia sheria na kanuni za TCRA lakini msisahau kuna teknolojia ambayo kwa sasa maroboti ndiyo yanatumika kutoa taarifa bila kumwona au kumfahamu mhusika. Sijui mmejipangaje kusimamia kanuni na kudhibiti ukiukwaji wa kanuni,” alisema.

Melo alisema TCRA ina wajibu wa kuhakikisha inakaa na wamiliki wa mitandao ya kijamii na ikiwezekana watu ambao wana wafuasi wengi kwenye mitandao  ili kupeana elimu kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui wa TCRA, Valerie Msoka, aliwataka wamiliki wa mitandao kuzingatia uchujaji wa habari wakati wa kuzichapisha.

“Ni wajibu wetu kufahamu si kila habari tunayoipata kutoka kwa jamii inafaa kusambazwa. Maadili ya uandishi tunayotumia na kuzingatia kwenye vyombo vya utangazaji wa redio na televisheni yanapaswa kutumika kwenye usambazaji wa habari kupitia mitandao. Tuelewe kuwa kuna habari zingine hazina tija kwa jamii na zingine huleta uchochezi,” alisema.

Pia aliwataka wamiliki hao kuzingatia faragha za watu binafsi na kwamba mambo ya kifamilia hayapaswi kusambazwa kwenye vyombo vya habari vya mitandaoni jambo ambalo linaondoa heshima ya mtu.

Msoka pia aliwataka kuzingatia matumizi ya lugha  na vyanzo na usambazaji wa habari na matukio.

 

Habari Kubwa