Temeke wataka Majaliwa asukume bn286/-

07Feb 2016
Moshi Lusonzo
Nipashe Jumapili
Temeke wataka Majaliwa asukume bn286/-

MADIWANI wa Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, wameunda timu maalumu kwa lengo la kukutana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aweze kusukuma utekelezaji wa mradi wa Sh. bilioni 286.

Akitoa tamko katika kikao cha madiwani kilichofanyika wilayani humo, Meya wa Manispaa hiyo, Abdallah Chaurembo, alisema mradio huo wa kuboresha makazi jijini Dar es Salaam (DMDP) una thamani ya Sh. bilioni 600, Temeke ikipewa mgawo wa asilimia 42 sawa na Sh. bilioni 266. Chaurembo, alisema wameamua kumuona Waziri Mkuu Majaliwa baada ya mradi huo kuchelewa kuanza licha ya Halmshauri hiyo kutimiza masharti ya kuwa na fedha za ulipaji fidia. Timu hiyo ambayo itaongozwa na yeye mwenyewe, watendaji na baadhi ya madiwani, itakuwa na jukumu la kuiomba serikali kuu kuharakisha mradi huo kwa manufaa ya wananchi. Alitaja sekta zitakazonufaika na mradi huo kuwa ni ujenzi wa barabara, uboreshaji wa makazi na ujenzi wa mifereji. Chaurembo alisema Manispaa ilichukua mkopo wa Sh. bilioni 19.6 kutoka benki ya CRB kwa ajili ya kulipa fidia kwa miradi itakayoanzishwa. “Sisi kama Halmashauri tupo tayari kuanza mradi huo, fedha zipo," alisema Chaurembo. "Tutakwenda kumuona waziri Mkuu ili mradi huo uanze mara moja.” Awali Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Photdas Kagimbo, alisema mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia utahusisha miradi 20 katika sekta tofauti. Aidha, Kagimbo alisema tayari fidia ya Sh. Milioni 700 imelipwa kwa wahusika kutoka mapato ya ndani ya Manispaa.

Habari Kubwa