Tewuta yaibukia sakata la Airtel

29Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Tewuta yaibukia sakata la Airtel

CHAMA cha Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mtandao na Mawasiliano (Tewuta) kimempongeza Rais Dk. John Magufuli  kwa kuitaka kampuni ya simu ya Airtel kuanza kuchunguzwa.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam,  Katibu Mkuu wa Tewuta, Junus Ndaro, alisema chama hicho kimefurahishwa na uamuzi wa Rais Magufuli kutaka kutatua suala hilo ambalo wamelilalamikia kwa muda mrefu.

Junus alisema uamuzi huo umewagusa Watanzania wengi hasa wafanyakazi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kwa kuwa imekuwa faraja kubwa kwao kwa kuleta matumaini mapya kwa kushudia kampuni yao iliyoanzishwa kwa mtaji na jasho lao, ikirejeshwa na kuwa mali ya umma.

“Tewuta kupitia kumbukumbu zetu za chama kwa miaka mingi tangu 2005, tuliwasilisha malalamiko yetu kutokana na kuporwa kwa TTCL lakini malalamiko hayakupata majibu. Tunamshukuru kwa dhati Rais Magufuli kuamua kufuatilia hili”, alisema Ndaro.

Alisisitiza kuwa kulikuwapo na mchezo uliosababishwa na Watanzania wachache wenye uchu wa fedha na wasiojali maslahi ya nchi yao, waliosaidiana na wawekezaji katika kupora rasilimali hiyo muhimu kwa taifa.

Aidha, chama hicho kinampongeza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL,  Omary Nundu, kwa kuwa tayari kuthibitisha uhalali wa kampuni ya simu ya Airtel.

Naye Mwenyekiti wa chama hicho, Pius Makuke, alisema TTCL haikuporwa kampuni ya Airtel pekee bali ilinyang’anywa pia Chuo cha Posta na Simu, kitendo ambacho kilisababisha wafanyakazi wake kukosa mahali sahihi kwa kupata mafunzo ya kujiendeleza kitaaluma.

“Mbali na pongezi hizo, tunazidi kuiomba serikali kukamilisha mchakato wa uchunguzi juu ya taarifa hizo pamoja na kufuatilia undani na kuzirejesha mali zote za TTCL  zilizoporwa kifisadi katika kipindi cha ubinafsishwaji kiwamo kilichokuwa Chuo cha Posta na Simu kilichoko kijitonyama jijini Dar es Salaam”, alisema Makuke.

TTCL ilibinafsishwa kwa mwekezaji wa nje mwaka 2001, wakati huo kampuni hiyo ilikuwa imeshaanzisha kampuni ya simu za mkononi iliyojulikana kama Celnet.

Baada  ya kuingia kwa wawekezaji, kampuni hiyo ilibadilishwa jina na kuitwa Celtel ambayo iliwezeshwa na TTCL kimtaji, kiufundi, kimiundombinu na hesabu zake zilikuwa zikikaguliwa pamoja.

Habari Kubwa