TFDA yajitosa kupambana uingizwaji chumvi isiyo na viwango

05Mar 2019
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
TFDA yajitosa kupambana uingizwaji chumvi isiyo na viwango

MAMLAKA ya Chakula na Dawa nchini (TFDA), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, imeanza kupambana na uingizwaji na uzalishaji wa chumvi ambayo haina madini joto ili kukabiliana na madhara ya udumavu kwa watoto.

Akizungumza wakati wa mafunzo, Meneja wa TFDA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Rodney Alananga, alisema matumizi ya chumvi hiyo yanasababisha madhara mbalimbali kwa wananchi ikiwamo udumavu wa watoto.

Alisema ili kupambana na hali hiyo wameanza kutoa mafunzo maalumu kwa maofisa lishe wa mikoa, wataalamu wa maabara za TFDA zilizoko kwenye mikoa yote na watumishi wengine wa mamlaka hiyo.

Alisema wameanza kutoa mafunzo kwa wataalamu hao ili kuongeza ukaguzi kwenye mikoa na wilaya zote za mkoa huo ili kuhakikisha matumizi ya chumvi hiyo yanakomeshwa na kuwaokoa wananchi na madhara ya chumvi hiyo.

Alananga alisema pia wanakusudia kuyatumia mafunzo hayo kuongeza idadi ya sampuli ya chumvi inayotumiwa na wananchi kwa kuikusanya kutoka kwa waingizaji wa chumvi, wauzaji na hata inayotumiwa na wananchi majumbani.

"Lengo la haya mafunzo ni kuhakikisha tunalinda afya za Watanzania, sasa tuna changamoto ya baadhi ya waingizaji wa chumvi na wazalishaji kuleta chumvi ambayo haina madini joto, sasa tunaamini haya mafunzo yatatusaidia," alisema Alananga.

Alisema wameamua kuimarisha mifumo ya ukaguzi ili kudhibiti wasambazaji wa chumvi na wazalishaji na kuhakikisha halmashauri zinaongeza ukaguzi wa chumvi.

Ofisa wa Mkoa wa Njombe, Willium Msenenda, alisema katika mkoa wa Njombe, Wilaya ya Wanging'ombe ndio yenye changamoto kubwa ya matumizi ya chumvi ambayo haina madini joto na hivyo kusababisha madhara.

Alisema wachimbaji hao wanatumia chumvi ya asili ambayo ina madini joto kidogo na inazalishwa katika mazingira ambayo usafi wake sio wa uhakika na hivyo inaweza kuwaletea madhara ya kiafya.

Alisema chumvi hiyo inachimbwa na wachimbaji wadogo katika wilaya hiyo na kusambazwa kwa wananchi ambao wanaitumia bila kujali madhara ya kiafya yanayoweza kuwakuta kutokana na matumizi ya chumvi hiyo.

"Tukiletewa ile chumvi ili tuipime kwenye maabara zetu tunakuta ina madini joto kidogo sana na hivyo haifai kwa matumizi ya binadamu, lakini wale wachimbaji wadogo wanaendelea kuizalisha na inatumiwa na wananchi," alisema Msenenda.

Kwa upande wake Mratibu wa Lishe wa Mkoa wa Mbeya, Benson Sang, alisema wapimaji wa sampuli ya chumvi wanakabiliwa na uhaba wa vitendea kazi vya kupimia chumvi hiyo hali inayosababisha kasi kuwa ndogo.

Alisema wakati mwingine vifaa hivyo huwa wanategemea wapewe na wafadhili hali ambayo inasababisha kuchelewa kupima na kwamba mpaka sasa kwenye halmashauri hakuna vipimo hivyo.

Habari Kubwa